Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Oktoba 22, 2025 anatarajiwa kuendelea na siku yake ya pili ya Kampeni Jijini Dar Es salaam, zamu hii ikiwa ni katika Wilaya ya Ilala, akitarajiwa kunadi Ilani ya Chama Chake, kueleza mafanikio ya Miaka yake minne madarakani katika kuwatumikia Watanzania na kuomba kura za wananchi kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 29.
Mkutano wa leo Jumatano, Wiki moja kamili kabla ya uchaguzi Mkuu wa Jumatano ya wiki Ijayo unatarajiwa kufanyika kwenye Kata ya Kinyerezi akitarajiwa kuzungumza na wananchi wa Majimbo ya Segerea, Ukonga na Kivule. Mkutano wa mwisho kwa Jiji hilo ukipangwa kufanyika kesho Alhamisi Wilayani Temeke na kuhusisha wananchi wa Majimbo ya uchaguzi ya Temeke, Mbagala na Chamazi.
Jana Jumanne Dkt. Samia akiwa Kwenye Mkutano wake wa kwanza Leaders Club Kinondoni pamoja na mambo mengine aliahidi kuanza na kukamilisha ujenzi wa barabara ya juu (Flyovers) kwenye Makutano ya Mwenge, Morocco, Magomeni na barabara za Ali Hassan Mwinyi, akisisitiza kuwa lengo ni kupunguza msongamano, kuongeza ufanisi wa barabara na kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii Mkoani humo.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia pia mbele ya maelfu ya wananchi wa Majimbo ya Kinondoni, Kibamba, Ubungo na Kawe, aliahidi pia kushughulikia maeneo yenye kukabiliwa na changamoto ya mafuriko Jijini Dar Es Salaam ikiwemo maeneo ya pembezoni mwa Mto Mbezi, Mto China na Mto Gide akisema Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) awamu ya pili utamaliza changamoto hiyo.
Kwa upande wa barabara, Dkt. Samia alisema ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, atakamilisha ujenzi wa barabara ya Kimara- Mavurunza- Bunyokwa- Kinyerezi, yenye urefu wa Kilomita saba, barabara muhimu kwa maendeleo ya Majimbo matatu ya Segerea, Kibamba na Ubungo, akiahidi pia upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki sehemu ya Kilomita tisa kutoka Morocco hadi Kawe na barabara ya Garden (Garden road) pamoja na barabara ya Tegeta- Bagamoyo yenye jumla ya urefu wa Kilomita 57.
Kwa Upande wa Ubungo Ilani anayoinadi Dkt. Samia imeahidi kuendeleza ujenzi wa barabara ya Kimara- Bonyokwa, Kisopwa- Kwembe- Makondeko na Kibamba- Magoe kwa kiwango cha lami, kutekeleza mradi wa Maji Msumi kutoka Tenki la Tegeta A, kujenga Vivuko vya Msewe, Sahara (Mabibo na Sahara (Mburahati) na ujenzi wa barabara za Goba Kinzudi, Goba Majengo, Konoike, Malamba Kingazi, Ufi Makaburini, Njeteni, Makabe na Azimio Kwembe kwa kiwango cha lami na barabara za King'ongo, Urassa, Kwa Msuguri, Mabibo Hostel, Tatedo, Makaburini, TAG Bethel na Msewe kwa kiwango cha Zege.
No comments:
Post a Comment