KAMPENI ZA DKT. SAMIA KUTIKISA MKOA WA MARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 9, 2025

KAMPENI ZA DKT. SAMIA KUTIKISA MKOA WA MARA


Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Oktoba 09, 2025 anatarajiwa kutikisa Mkoani Mara, kwenye muendelezo wa Kampeni zake, wananchi wakieleza kumsubiri kwa shauku kama dhihirisho la ahsante kwa maendeleo aliyowaletea Mara.

"Wananchi na Wanachama wa CCM tumejipanga kumpokea kwa Kishindo kikubwa na sababu za kumpokea tunazo, amefanya kazi yake vyema na ametekeleza Ilani kwa zaidi ya asilimia mia moja na Ilani aliyoiandaa kwasasa inagusa maisha ya wananchi kwahiyo tunayo hamu sana ya kumuona na kumsikiliza Mgombea Urais huyu ambaye ametujengea pia Hospitali ya Rufaa na zaidi ametujengea Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, chuo hiki kimetupa heshima watu wa Mara."- Amekaririwa akisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Ndugu Patrick Chandi.

Dkt. Samia anaanza kampeni zake Mkoani humo akisifika kwa kuidhinisha zaidi ya shilingi Trilioni 1.3 kutekeleza miradi ya maendeleo katika Miaka yake minne madarakani, wakiongeza Vituo vya afya kutoka 42 hadi 56, Zahanati kutoka 263 hadi 333 na Hospitali za Halmashauri kutoka 11 hadi kufikia 20, akipeleka huduma za Kibingwa za Matibabu pia Mkoani humo ikiwemo pua, sikio na koo, kuzalisha gesi tiba ya Oksijeni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu kimkoa kutoka asilimia 80.4 hadi asilimia 84.9.

Aidha kulingana na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya 2020/25, Mkoa huo pia umefanikiwa kuongeza idadi ya Viwanda vidogo, vya kati na Vikubwa kutoka Viwanda 90 mwaka 2020 hadi Viwanda 319, kuongeza mtandao wa barabara za lami kutoka Kilomita 293 hadi 407, barabara za Changarawe kutoka Km 1399 hadi 2,425 pamoja na kuongeza kiwango cha Mikopo kwa wanawake, Vijana na wenye ulemavu kutoka Shilingi Bilioni 1.63 hadi kufikia Bilioni 5.88.

No comments:

Post a Comment