KOMBO AHIMIZA TCCIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 22, 2025

KOMBO AHIMIZA TCCIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amezindua Mkutano Mkuu Maalum wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kuwa injini kuu ya kuimarisha diplomasia ya uchumi nchini.

Mhe. Kombo amesema licha ya mchango wake mkubwa katika kukuza biashara, TCCIA imepoteza fursa muhimu za kimataifa, hivyo ni wakati muafaka kwa taasis hiyo kujipanga upya ili kuwa daraja madhubuti kati ya sekta binafsi na Serikali kwa kuvutia uwekezaji, kutengeneza ushirikiano wa kimataifa, kukuza masoko ya bidhaa nje ya nchi na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa.

Aidha, ameitaka TCCIA kuwa mshauri wa Serikali katika kukuza biashara za kimataifa, kuongoza safari za wafanyabiashara nje ya nchi, na kutoa taarifa sahihi za masoko ya kimataifa. Amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na TCCIA kupitia jukwaa la diplomasia ya uchumi ili kuiunganisha na majukwaa ya kimataifa ya biashara na uwekezaji.

Vilevile, ameipongeza TCCIA kwa hatua ya kuboresha Katiba yake na kuwataka viongozi wake kuimarisha nafasi ya taasisi hiyo katika utendaji wa diplomasia ya uchumi, akibainisha kuwa sekta binafsi ndiyo injini kuu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Kombo ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na TCCIA katika utekelezaji wa mikakati ya kukuza uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi na hatimaye akafungua rasmi Mkutano Mkuu Maalum wa TCCIA Taifa.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, amesema mkutano huo Pamoja na mambo mengine, ulipitia na kuboresha katiba ya chemba hiyo, ili kuifanya iendane na mahitaji na mabadiliko ya sasa.

Bw. Minja ameongeza kuwa mchakato huo unalenga kuhakikisha ushiriki mpana na jumuishi, hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya TCCIA.





No comments:

Post a Comment