
Mavunde ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 12, 2025 mbele ya Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa kampeni za Dkt. Samia kwenye Viwanja vya Shule ya msingi Ushirombo Wilayani Geita,akisema hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa Rais Samia kutaka Vijana waliokuwa wakichimba madini hayo kinyemela kutaka warasimishwe na wawezeshwe kuweza kuvuna rasilimali hiyo ndani ya pori hilo.
Amemueleza Dkt. Samia pia kuhusu utekelezaji wa maelekezo yake, akisema tayari Wizara yake na Wizara ya Maliasili na Utalii zinaendelea na Vikao vyake ili kuboresha zaidi mazingira ya wachimbaji wadogo ndani ya pori hilo la akiba, kwa lengo la kuondoa changamoto za kisheria.
"Dkt. Samia pia umetuelekeza matamanio yako ya kuona Watanzania wengi zaidi wananufaika na kuona mabilionea wengi zaidi wanatengenezwa. Maelekezi yako ni kuwa Benki kuu ya Tanzania na Wizara ya fedha kupitia mfuko wa dhamana watenge fedha na waanze kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wamiliki migodi na waweze kununua madini nchini badala ya kupelekwa Dubai." Amesema Waziri Mavunde.
Mavunde kadhalika ametoa rai kwa wananchi wote wa Geita kujitokeza kwa wingi kumpa kura za kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan hapo Oktoba 29, 2025, akimshukuru pia kwa kufanikisha ujenzi wa masoko 2 na Vituo viwili vya madini kwa Wilaya ya Bukombe pamoja na utoaji wa mashine moja ya kuchoronga iliyokabidhiwa kwa wachimbaji wadogo wa madini wa pori la akiba la Moyowosi/ Kigosi.





No comments:
Post a Comment