MALIASILI YAJIPANGA KUANDAA MPANGO MKAKATI ENDELEVU 2025/26 – 2030/31 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 21, 2025

MALIASILI YAJIPANGA KUANDAA MPANGO MKAKATI ENDELEVU 2025/26 – 2030/31



Na Sixmund Begashe, Dodoma


WIZARA ya Maliasili na Utalii imejidhatiti kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na uelewa mpana kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2025/26 – 2030/31, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha utendaji na kufikia malengo ya sekta kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha tathmini kilichofanyika jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bernard Patrice Marcelline, amesema Wizara hiyo ina wajibu mkubwa wa kusimamia uhifadhi wa maliasili na kukuza utalii nchini, hivyo ni muhimu kwa watumishi wake kuwa na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa mpango huo.

“Wizara imejipanga kuhakikisha watumishi wote wanajengewa uwezo ili waendane na kasi ya utekelezaji wa Mpango Mkakati uliopo na ule ujao. Lengo ni kuhakikisha tunafikia malengo ya maendeleo na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa,” amesema Marcelline.

Aidha, amewapongeza washiriki wa kikao kazi hicho kwa ushiriki wao na kuwataka kuyafanyia kazi mapendekezo na maazimio yaliyotolewa, kwa manufaa ya umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Abdallah Mvungi, amesema Idara yake itaendelea kutoa mafunzo na warsha mbalimbali kwa watumishi kutoka Idara na Vitengo tofauti, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara, unaolenga kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na ubunifu katika sekta ya maliasili na utalii nchini.


No comments:

Post a Comment