Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi ameongoza ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 19 wa Kati wa Mawaziri wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) unaofanyika jijini Kampala, Uganda.
Mkutano huo unaofanyika tarehe 15-16 Oktoba ,2025 ulitanguliwa na kikao cha ngazi ya wataalam kilichofanyika tarehe 13–14 Oktoba 2025.
Mkutano huu wa NAM unajadili mbinu za kukabiliana na changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazoyakabili mataifa wanachama katika mazingira ya sasa ya dunia.
Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri Chumi amezisihi nchi za NAM kuendeleza mshikamano na umoja katika majadiliano ya kimataifa, hasa katika kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea.
Aidha, alisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kulinda na kutetea maslahi ya pamoja ya umoja huo.
Mkutano huo unatarajiwa kupitisha Azimio la Mwisho la Kampala pamoja na Tamko kuhusu Palestina, likiwa ni sehemu ya matokeo ya majadiliano yanayolenga kuimarisha nafasi ya NAM katika masuala ya kimataifa.
Mkutano wa mwaka huu umefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, ambaye alisisitiza umuhimu wa mshikamano, ushirikiano na utetezi wa maslahi ya nchi zinazoendelea ndani ya mfumo wa kimataifa.
Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) una wanachama 120, ulianzishwa wakati wa enzi za Vita Baridi kwa lengo la kusaidia nchi kutoka Asia, Afrika na Amerika ya Kusini kuondokana na ukoloni na kujijengea uwezo wa kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment