SERIKALI NA VIETTEL GLOBAL WASAINI MAKUBALIANO MAPYA KUENDELEZA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 6, 2025

SERIKALI NA VIETTEL GLOBAL WASAINI MAKUBALIANO MAPYA KUENDELEZA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO


Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikia makubaliano mapya na kampuni ya VIETTEL Global kuendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano nchini, baada ya kutatua changamoto zilizojitokeza katika mkataba wa awali uliosainiwa mwaka 2014.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kampuni hiyo kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yaliyo nje ya mkataba bila idhini ya Serikali pamoja na kutotekeleza kikamilifu jukumu la kufikisha huduma hiyo katika maeneo yenye uhitaji zaidi ndani ya Tanzania.


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba wa nyongeza wa utekelezaji wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (GNT) ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Adolf Ndunguru, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha makosa ya awali hayajirudii na wananchi wote wananufaika na uwekezaji huo mkubwa.

“Makubaliano haya mapya yamekuja baada ya serikali kubaini mapungufu yaliyokuwepo katika mkataba wa awali. Tumekubaliana kwa pamoja kuweka utaratibu thabiti wa usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha malengo ya serikali ya kufikisha mawasiliano kwa wote yanatimia,” alisema Ndunguru.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mkataba wa awali ulioingiwa mwaka 2014 ulikuwa wa miaka 25 kati ya serikali na kampuni ya VIETTEL Global, wamiliki wa mtandao wa mawasiliano wa Halotel, kwa ajili ya kutekeleza Awamu ya Nne ya Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Awamu hiyo inalenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi hasa katika maeneo ambayo hayakunufaika katika awamu zilizopita za mradi huo.

Upande wa serikali uliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, ambaye alisema kusainiwa kwa mkataba huo mpya ni ushahidi wa dhamira ya serikali kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika kukuza huduma za TEHAMA nchini.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji wenye nia njema kama VIETTEL Global kuhakikisha teknolojia ya mawasiliano inawafikia Watanzania wote, mijini na vijijini, kwa gharama nafuu na kwa ubora wa kimataifa,” alisema Abdulla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VIETTEL Global, Bi. Nguyen Thi Hoa, alisema kampuni hiyo imejifunza kutokana na changamoto zilizopita na imejipanga upya kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa uwazi, kasi na ubora unaotarajiwa.

“Tumejipanga kuboresha utendaji wetu na kushirikiana kwa karibu na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kila hatua ya mradi inatekelezwa kwa ufanisi. Tumejizatiti kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyotengwa,” alisema Bi. Hoa.

Makubaliano hayo mapya yanatarajiwa kuimarisha upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti, simu na data, pamoja na kuimarisha mifumo ya kidijitali katika sekta mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment