TFRA yaadhimisha Siku ya Mbolea Duniani kwa namna yake - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 13, 2025

TFRA yaadhimisha Siku ya Mbolea Duniani kwa namna yake


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ujindile, kata ya Igosi, wilayani Wanging’ombe, mkoani Njombe Katika maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yaliyoadhimishwa kitaifa mkoa wa humo, tarehe 13 Oktoba, 2025.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, Samson Kapange, akitoa salamu za shukrani kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kuamua kufanya Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani katika wilaya anayoisimamia na kueleza I am manufaa makubwa kwa wakulima wa kijiji cha Ujindile na Kata nzima ya Igosi.


Na Mwandishi Wetu, Njombe


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent amewasihi wakulima kuhuisha taarifa zao za mashamba katika mfumo wa usajili wa wakulima ili kuwawezesha kupata mbolea kulingana na uhitaji wao kwa kuwa wakulima hao wanakuwa shambani kwa mwaka mzima katika maeneo wanayolima.

Ametoa wito huo kwa wakulima wa Kijiji cha Ujindile Kata ya Igosi mkoani Njombe ambapo hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani kwa mwaka 2025 yamefanyika.

Ameeleza pia kuwa lengo kuu la kuwepo ni kubadilishana uzoefu kati ya wakulima, wataalamu na wazalishaji na waingizaji wa mbolea ili kuongeza tija katika shughuli za kilimo.
“Kuna maeneo maalum kama Mamlaka tumeona ni vyema kuyatazama upya.

Tumeongeza idadi ya mifuko ya mbolea kwenye eneo la viazi, na tumeanza kuona vijana wakijitokeza zaidi kutokana na tija wanayoiona kwenye kilimo.

Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima jirani na mashamba yao,” amesema Laurent.

Aidha, amewasihi wakulima kupima afya ya udongo ili waweze kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na aina ya zao wanalolima.

“Uwezo wa uzalishaji wa mbolea kwa makampuni ya ndani umeongezeka kutoka tani 100,000 mwaka 2023 hadi kufikia tani 250,000 mwaka huu wa 2025 kwa kiwanda cha Minjingu huku kiwanda cha Itracom kilichopo Nala jijini Dodoma, kikiongeza uwezo wake kutoka tani 200,000 hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu,” amesema Laurent.

Akieleza mwitikio wa wakulima kwenye matumizi ya Mbolea nchini, Mkurugenzi Mtendaji Joel amesema matumizi yameongezeka kutoka tani 365,000 mwaka 2022/2023 na kufikia tani 974,000 mwaka 2024/2025 huku matarajio ni kiasi hiki kuongezeka kila mwaka na kwa mwaka 2025/26 tunatarajia matumizi yatafika tani 1,100,000 na mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila kata nchini inakuwa na angalau wakala mmoja wa mbolea.

Ameongeza kuwa, matumizi sahihi ya mbolea yatapelekea kufikiwa kwa malengo ya Agenda 10/30: Kilimo ni Biashara mara baada ya kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa wakulima, na kuwafanya wakulima kuongeza tija na kulima kibiashara na hivyo kukuza uchumi wa kaya zao na taifa kwa ujumla na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Tunataka wakulima waendelee kupima afya ya udongo, kutumia mbolea kwa usahihi na kulima kwa tija.” amesema Laurent.

Kwa upande wake, Heri Chengula mkulima wa parachichi kutoka kijiji cha Ujindile, ameishukuru Serikali kupitia TFRA kwa kuendelea kuwezesha wakulima kupata mbolea za ruzuku kwa urahisi zaidi.

“Mbolea za ruzuku zimetupa unafuu mkubwa sana na uzalishaji wa mazao ya mahindi umeongezeka kutoka kuvuna gunia moja hadi 15 baada ya kuanza kutumia mbolea za viwandani,” amesema Chengula.

“Tunaendelea kujifunza kuhusu namna sahihi ya kutumia mbolea kwenye mazao mbalimbali, na tunashukuru kwa juhudi za TFRA kutusogezea huduma hizi karibu,” ameongeza Mwalongo.

Kwa mwaka huu 2025 Mamlaka imeadhimisha Siku ya Mbolea Duniani kwa kupeana uzoefu na wakulima na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga, Rukwa na Manyara, Kagera na elimu hii inaendelea nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Mali shambani, Silaha Mbolea.

Mkulima Bisheni Msaya kutoka kijiji cha Ujindile akitoa ushuhuda wa mafanikio aliyofikia baada ya kuzingatia kanuni za matumizi sahihi ya mbolea kwa kuanza na zoezi la kupima afya ya udongo na kutumia mbolea kulingana na ushauri wa kitaalam alioupata na hivyo kuongeza mavuno kwa kiwango kikubwa.

Ametoa ushuhuda huo tarehe 13 Oktoba, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Dunia yaliyofanyika katika kijiji hicho kata ya Igosi wilaya ya Wangong'ombe mkoani Njombe





Wananchi wa kijiji cha Ujindile, kata ya Igosi, wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, wakifuatilia mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea kutoka kwa wataalam wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yaliyoadhimishwa kitaifa mkoani Njombe kwa mwaka 2025.

Hafla hiyo imewakutanisha watumishi kutoka Wizara ya Kilimo, wazalishaji wa mbolea, kampuni za mbolea nchini watumishi kutoka ngazi ya mkoa, wilaya na kata na vijiji vya mkoa wa Njombe na Wilaya ya Wanging'ombe tarehe 13 Oktoba, 2025

No comments:

Post a Comment