
Na : Dickson Bisare- Dar Es Salaam
Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeshika kasi katika Jimbo la Mbagala baada ya viongozi na wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani kuwasili katika ofisi za chama tawi la Changanyikeni, Kata ya Toangoma, kwa ajili ya kuomba kura kwa wananchi.
Katika mkutano huo, mgombea wa nafasi ya Udiwani Kata ya Toangoma, ndugu Msigwa, alisimama mbele ya wananchi na kuwaomba kura ili aweze kuwa mwakilishi wao. Msigwa aliwaahidi wananchi kuwa pindi wakimchagua, maendeleo zaidi yatafuata hatua kwa hatua.
Sambamba na hilo, mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Mbagala, ndugu Kakulu Burchad Kakulu, alieleza kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya ubunge, atahakikisha barabara zote korofi kuanzia maeneo ya Maliasili hadi Changanyikeni zinakarabatiwa. Aidha, aliahidi kufanikisha ujenzi wa kituo cha afya chenye hadhi kubwa katika mtaa wa Malela ili kuboresha huduma za afya.
Mbunge mtarajiwa huyo pia aligusia changamoto za ajira kwa vijana waliomaliza vyuo bila kupata kazi. Alisema akichaguliwa atazindua programu maalum za ujuzi zitakazowezesha vijana kujiajiri kupitia miradi ya viwanda vidogo, ikiwemo kuchakata nyama za kuku na kuvutia wawekezaji kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wa wanawake, Kakulu aliahidi kupigania upatikanaji wa mikopo kwa urahisi zaidi ili kuwawezesha kina mama kuanzisha na kukuza biashara zao. Alisisitiza kuwa CCM ndicho chama kinachoweza kutimiza matamanio ya wananchi na kuwaletea maendeleo ya kweli.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa mtaa wa Changanyikeni, ndugu Shabani Mgodoka, aliwahimiza wananchi kuhakikisha tarehe 29 Oktoba 2025 wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura za Ubunge kwa ndugu Kakulu Burchad Kakulu na Udiwani kwa ndugu Msigwa kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Mkutano huo ulihitimishwa na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Changanyikeni, ndugu Alex Marindo, ambaye aliwaomba wananchi waendelee kukiamini na kukichagua CCM katika nafasi zote, kuanzia Rais, Mbunge na Diwani, kwa ajili ya kuendeleza misingi ya maendeleo.




No comments:
Post a Comment