Na Mwandishi Wetu, Tabora
VIONGOZI wa dini katika mikoa ya Kanda ya Magharibi wameazimia kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao uliopangwa kufanyika oktoba 29, 2025.
Kadhalika viongozi hao kutoka mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi wamesisisitiza umuhimu wa kutumia nyumba za ibada kuhubiri amani na kuwakemea wote wanaotaka kuvuruga utulivu wa nchi.
Wakizungumza kwenye kongamano la Amani na Uchaguzi lililofanyika leo oktoba 24, 2025 mkoani Tabora, viongozi hao pia wametoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura kwani ni haki yao kidemokrasia.
Katika maazimio waliyoyasoma mwishoni mwa kongamano hilo viongozi hao wa dini wamesisitiza ulinzi wa amani ya nchi na hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Akisoma maazimio hayo, Katibu wa CPTC Mkoa wa Tabora, Mchungaji Lameck Hazina amesema wamekubaliana kuendelea kuelimisha waumini kuepuka kushiriki maandamano au vitendo vyote vinavyoweza kuvuruga uchaguzi na kuhatarisha amani ya nchi.
“Tumeazimia kwamba viongozi wa dini hatupaswi kwa namna yoyote kuhamasisha vurugu, bali tuwe chachu ya amani, upendo na umoja miongoni mwa Watanzania wote,” amesema.
Aidha, viongozi hao wamekumbusha waumini kwamba dini zote zinahimiza kutii mamlaka kwa kuwa viongozi hutoka kwa Mungu, hivyo ni wajibu wa wananchi kuwaheshimu na kuwaombea wawe waadilifu katika uongozi wao.
Mapema akifungua kongamano hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ibrahim Mavumbi, amesema Watanzania wanapaswa kuwa waangalifu kuelekea uchaguzi ili kuepuka kugawanyika kwa misingi ya kisiasa au kikabila.
“Tusiposhikana na kulinda amani tuliyorithishwa na waasisi wetu akiwemo Hayati Mwalimu Julius Nyerere, taifa linaweza kuingia kwenye sura mbaya. Bila amani hakuna maisha, tusikubali kuingizwa katika migawanyiko kupitia vyama vya siasa,” amesema Sheikh Mavumbi.
Amesisitiza kuwa makongamano ya aina hiyo yasifanywe tu wakati wa uchaguzi, bali yaendelee mara kwa mara ili kukuza utamaduni wa amani nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa Kadhi Mkoa wa Mwanza, Sheikh Ramadhani Khamis, amesema mafundisho ya Kiislam yanawataka waumini kuwa na amani na kuheshimu mamlaka, akiwataka viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kukemea wale wote wanaopanga vurugu.
“Wapo watu wanaoitakia nchi yetu mabaya, tunapaswa kuwakemea kwa nguvu zote kwa sababu wengi wao ni waumini wetu wanaokuja katika nyumba za ibada,” alisema Sheikh Khamis.
Askofu Denis Michael Nkwera, kutoka Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPT), ametoa tahadhari kwa Watanzania kuilinda amani iliyopo akisema, “Iwapo vurugu zitatokea, Watanzania tutakimbilia wapi? Wenzetu wa Rwanda, Kongo na Kenya wanatamani kukimbilia Tanzania kwa sababu ya amani tuliyonayo.”
Ameongeza kuwa, “Mtanzania halisi hawezi kuhamasisha vurugu katika nchi hii ambayo Mungu ametubariki amani. Tuitunze na tuishikilie kwa wivu mkubwa.”
Sheikh wa Shia Mkoa wa Tabora, Swahibu Shaban amesema suala la amani ni pana na linapaswa kufundishwa tangu elimu ya awali ili watoto wajue thamani ya amani.
Naye Mchungaji Edward Kadangi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Wilaya ya Urambo, amesema vitabu vyote vya dini vimehimiza amani, na kwamba wale wanaotaka kuvuruga amani “hawana dini.”
“Hata kama jambo haliko sawa, sio lazima uharibu amani. Tunapoelekea uchaguzi twende kwa amani na tubaki na amani hata baada ya uchaguzi,” amesema Kadangi.
Kwa upande wake, Sheikh Iddy Suleiman ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Wilaya ya Igunga, amewaasa wananchi kuwa wavumilivu wanapohisi kunyimwa haki, badala ya kutumia maandamano, wamuombe Mungu awape haki kwa njia ya amani.
Aidha, Mchungaji Meliciana Mivuko, amesema wanawake ndiyo wanaoteseka zaidi pindi migogoro au vita inapotokea, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda amani aliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa.
“Watumishi wa Mungu tuendelee kuombea nchi yetu kila siku, najua wapo watu wasiopenda mema kwa taifa letu, lakini jukumu letu ni kulinda amani na umoja wetu,” amesema.
Mwisho wa kongamano hilo, viongozi hao walikubaliana kuwa watatumia majukwaa yote ya dini kuhubiri amani, upendo na mshikamano kuelekea na baada ya Uchaguzi Mkuu.
























No comments:
Post a Comment