
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
VIONGOZI wa dini nchini wameendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na uzalendo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa ustawi wa taifa na ibada halisi kwa Mungu.
Wakizungumza leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, katika Kongamano la Amani la Kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu, lililofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, viongozi hao wamesema jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania, bila kujali dini wala itikadi.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuberi, amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na amani, upendo na uzalendo, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
“Sisi kama viongozi wa dini tunalazimika kufanya kazi waliyofanya mitume kuhakikisha amani inakuwepo ulimwenguni. Ukiwa na uzalendo utatunza amani, na kutunza amani ndiyo dini,” amesema Sheikh Mkuu.
Ameeleza kuwa makongamano ya amani yaliyofanyika katika kanda mbalimbali za nchi yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakumbusha Watanzania juu ya wajibu wa kulinda amani na kuendeleza mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Chesco Msaga, amesema amani ya kweli huanzia ndani ya moyo wa mtu binafsi kabla ya kuonekana katika jamii.
“Amani ya kweli inaanzia ndani ya roho. Kama sina amani moyoni siwezi nikapeleka amani kwa mtu mwingine,” amesema.
Mkurugenzi wa Al Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki, amewataka Watanzania kuendelea kulitetea taifa kwa maneno na matendo ya kizalendo, akisema ni kosa kwa mtu kutaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha maoni binafsi.
“Siku hizi ukisimama kulitetea taifa lako unaambiwa umepewa bahasha. Lakini nataka kuuliza, wale wanaotaka kuvunja amani wanapewa na nani?” amehoji.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Tanzania (JMAT-TAIFA), Alhad Mussa Salum, ametoa wito kwa wazazi na viongozi kuendelea kuwaelimisha vijana, hasa wa kizazi cha Gen Z, juu ya thamani ya nchi na madhara ya vurugu.
“Changamoto hazitatuliki kwa uharibifu bali kwa utaratibu. Tuwasihi vijana wetu kwamba kuiharibu nchi kisha kufikiria kuitengeneza upya si jambo la busara,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (CPCT), Dk. Vernon Fernandes, amesema rasilimali na mafanikio yaliyopo nchini hayawezi kudumu bila uwepo wa amani, akiwataka wananchi kujitokeza kupiga kura kwa utulivu.
Wakati huo huo, Serikali imetoa shukrani kwa viongozi wa dini kupitia Kamati ya Amani kwa juhudi zao za kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, wakati wa kufunga kongamano hilo, amesema makongamano ya amani yamekuwa chachu ya kuimarisha imani ya wananchi kuelekea uchaguzi.
“Tafiti zinaonyesha wananchi wengi wanawaamini zaidi viongozi wa dini wanapokuwa na changamoto zao. Kwa hiyo mchango wenu ni mkubwa sana katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki uchaguzi kwa amani,” amesema Prof. Mkumbo.
Ameongeza kuwa huu ni uchaguzi wa 14 tangu Tanzania ianze mfumo wa vyama vingi, hivyo ni kipindi muhimu cha kuendelea kudumisha amani kama urithi wa taifa.
Kongamano hilo limehitimisha mfululizo wa makongamano ya amani yaliyofanyika nchini kupitia kanda zote Kusini, Kaskazini, Kati, Magharibi na Nyanda za Juu Kusini yakiratibiwa na Kamati ya Amani ya Kitaifa.






No comments:
Post a Comment