Wasanii wa Muziki na Filamu waliojumuika na Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Oktoba 28, 2025 kwenye Viwanja vya michezo vya CCM Kirumba Mkoani Mwanza, wakiwa wanasoma machapisho mbalimbali ya mafanikio yaliyopatikana kwenye Miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa yaliyozungumzwa kama sehemu ya mafanikio ni katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini, ambapo katika kipindi kifupi cha miaka minne, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa SGR imeendelea kwa kasi ikiwa ni pamoja na kukamilisha kipande cha reli hiyo kutoka Jijini Dar Es Salaam hadi Mkoani Dodoma suala ambalo linatajwa kurahisisha usafiri, kupunguza muda wa safari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma pamoja na kusisimua shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kulingana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) hadi sasa zaidi ya abiria Milioni 3.8 wamesafirishwa na reli hiyo na wakiingiza zaidi ya shilingi bilioni 59 kama mapato tangu kuanza kwa uendeshaji wa reli hiyo kati ya Dar es salaam hadi Dodoma mnamo Juni 14, 2024 na Dar es salaam hadi Morogoro Julai 25, 2024 huku pia faida nyingine zikiwa ni kupatikana kwa usafiri na usafirishaji wenye staha na gharama nafuu,upunguza muda wa safari, uendeshaji wa reli ya SGR bila ruzuku ya Serikali, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na upatikanaji wa ajira ambapo ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,880 zisizo za moja kwa moja zimezalishwa kupitia miradi hiyo.
Mafanikio mengine ni utunzaji wa mazingira ambapo takribani tani 14,327.3 za hewa ya ukaa zimepungua, kusafirisha mzigo mkubwa kwa mara moja ambapo treni moja ina uwezo wa kubeba kiasi cha tani 3,000 kwa wakati mmoja, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara kutokana na mzigo mkubwa kusafirishwa kwa njia ya reli, kuchangia ufanisi wa bandari na ukuaji wa sekta zingine pamoja na kuchagiza ukuaji wa miji katika maeneo yaliyopo katika ushoroba wa reli.
Katika ahadi za Dkt. Samia kuelekea mwaka 2030, ameahidi ujenzi wa reli ya Kisasa Mwanza- Isaka (Km341), Makutupora- Tabora (Km368), Tabora- Isaka (Km165), Tabora- Kigoma (Km506) na Uvinza- Msongati (Km156.6) pamoja na kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya kuunganisha Bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musomaz itakayokuwa na urefu wa Kilomita 1, 108.
Mapema leo pia Mgombea Ubunge wa Arusha Mjini Paul Makonda amezungumzia uendeshaji wa Treni hizo za kisasa na kulisifu shirika la reli nchini kwa usimamizi mzuri wa utoaji wa huduma pamoja na hatua za haraka zinazochukuliwa pale ambapo kumekuwa kukitokea kwa hitilafu katika vyombo hivyo vya usafiri ikiwemo ajali ya Wiki iliyopita ya Mabehewa mawili kupinduka.









No comments:
Post a Comment