
Na Witness Masalu- WMJJWM- Iringa.
Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wana jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa jamii inaishi katika maadili ikiwemo kuzingatia mila na desturi za kitanzania zinazofaa.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu alipotembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha leo tarehe 16 Oktoba, 2025 mkoani Iringa.
Felister ameeleza kuwa nidhamu katika jamii haipo tena na wimbi la mmomonyoko wa maadili limekua kubwa kwani vijana hawana hofu ya kutumia lugha zisizofaa hadharani na kwenye mitandao ya kijamii hata kwa watu waliowazidi umri .
“Jamii zetu sasa hivi zinakwenda kinyume na maadili ya kitanzania kwani tunaona kwenye mitandao ya kijamii vijana wakitukana ovyo bila kujali na hiki ni kiashiria kuwa kuna shida sehemu hivyo basi Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wana jukumu la kufanya tafiti na kuja na majibu yenye suluhisho ili kutokomeza mmonyoko wa maadili” amesema Felister.
Vilevile Felister amekipongeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha kwa kazi nzuri inayokifanya kwa kuwainua mabinti wa kike na kuwajengea uwezo wa kujikomboa kiuchumi ikiwemo kushona cherehani na stadi nyingine za maisha.
“Mabinti hawa wanachukua kozi ya miezi sita na baada ya muda huo wanaenda mtaani kujitegemea hivyo basi nimefurahishwa na juhudi zao na nimetoa ahadi kuwa Wizara itawaongezea cherehani mbili ili waweze kuongeza nguvu “amesema Felister.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike amesema Serikali inapambana kuhakikisha Vyuo hivyo vya kati vinatoa mafunzo stahiki kwa wanafunzi na kunufaisha jamii za sehemu husika kupitia afua mbalimbali hivyo itaendelea kuvisimamia na kuvijengea uwezo.
Halikadhalika, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha Godfrey Mafungu ametoa pongezi kwa Serikali hususani Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kutenga muda wao kukagua mafunzo na miradi inayotekelezwa na Chuo hicho ili kuweza kuwajengea uwezo zaidi na kuhakikisha mambo yote yako sawa.


No comments:
Post a Comment