
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi CHICO anayejenga daraja la Nzali lenye urefu wa mita 60 na barabara unganishi km 1.5 wilayani Chamwino kukamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi ujao.
Akizungumza wakati akikagua miradi ya barabara mkoani Dodoma Mhandisi Kasekenya ameelezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hilo ambalo litaimarisha mawasiliano kati ya Kijiji cha Chilonwa na Nzali Wilayani Chamwino.
"Wananchi daraja hili sio la Serikali ni lenu hivyo litunzeni ili lidumu kwa muda mrefu epukeni kulima na kuchota mchanga karibu na daraja", amesisitiza Kasekenya.
Amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwenye ujenzi wa miundombinu hivyo kuwataka TANROADS kumsimamia vizuri mkandarasi ili mradi uwiane na thamani ya fedha.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Dodoma mhandisi Zuhura Amani amesema kukamilika kwa daraja hilo kutamaliza changamoto ya mawasiliano ya muda mrefu katika barabara ya Chamwino- Dabalo Itiso -Chinene Km 70 ambayo inaunganisha barabara ya Morogoro na Arusha na hivyo kuchochea shughuli za kilimo na biashara.
Zaidi ya shilingi bilioni 14.5 zimetumika katika ujenzi huo hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wilayani Chamwino.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (outer ring road) yenye urefu wa km 112.3 na kuwataka wakandarasi CCECC anayejenga sehemu ya kwanza Nala-Veyula-Ihumwa km 52.3 na Avic anayejenga sehemu ya pili Nala-Matumbulu-Mtumba km 60 kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati na hivyo kupunguza msongamano.
Aidha amehimiza bidii katika uwekwaji wa alama za barabarani, taa na upandaji wa miti kwaajili ya kupendezesha barabara hiyo.
Kukamilika kwa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma kutapunguza msongamano na kuchochea uchumi jijini Dodoma.






No comments:
Post a Comment