DKT. NCHEMBA: NITASHUGHULIKA NA WATUMISHI WAVIVU KWA FYEKEO NA RATO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 13, 2025

DKT. NCHEMBA: NITASHUGHULIKA NA WATUMISHI WAVIVU KWA FYEKEO NA RATO



Na OKULY JULIUS , Dodoma


Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema ataanza kazi kwa kasi kubwa ya kusimamia utendaji wa Serikali na kuhakikisha kila ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania inatekelezwa kikamilifu.

Akihutubia Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Kwanza, Kikao cha Tatu, leo Novemba 13, 2025 jijini Dodoma, Dkt. Nchemba amesema hatavumilia uvivu, uzembe, rushwa na lugha mbaya kwa wananchi miongoni mwa watumishi wa umma, akisisitiza kuwa “nakuja na fyekeo na rato.”

“Kwa watumishi wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania, tuwe tayari, nitakuja na fyekeo na rato. Lazima maono ya Mheshimiwa Rais na ahadi zake kwa Watanzania zitekelezwe,” alisema Dkt. Nchemba huku akishangiliwa na wabunge.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM imebeba masuala yote ya msingi yatakayosaidia kutatua kero za wananchi na kuleta matumaini mapya kwa Watanzania.

Dkt. Nchemba amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta za miundombinu, nishati, afya na elimu.

Amesema vijiji vyote nchini vimeunganishwa umeme na kazi iliyosalia ni kumalizia vitongoji, sambamba na utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya kutoa ajira milioni nane kwa vijana kupitia Ilani ya CCM.

Aidha, Waziri Mkuu Mteule huyo amesema Serikali itatekeleza mkakati wa kitaifa wa kuondoa umaskini, ambapo watumishi wa umma watapaswa kushuka hadi ngazi za chini kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050, Dkt. Nchemba alisema dira hiyo imebeba matumaini makubwa ya Watanzania, hasa vijana, na kwamba Serikali itaanza utekelezaji wake kwa kasi huku ikimalizia viporo vya dira iliyopita.

Pia alieleza kuwa kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kumemaliza changamoto ya kukatika kwa umeme nchini na kuifanya Tanzania kuwa na ziada ya umeme.

Kuhusu sekta ya afya, Dkt. Nchemba alisema Serikali imejenga zaidi ya hospitali 119 za wilaya, vituo vya afya 649 na zahanati 2,800, hatua iliyosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Katika sekta ya elimu, amesema ndani ya kipindi kifupi, shule mpya 2,700 za msingi na sekondari 1,300 zimejengwa pamoja na madarasa zaidi ya 97,000 nchi nzima, ikiwa ni juhudi za Rais Samia kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Rai yangu kwa Watanzania wote ni kuendelea kumtanguliza Mungu katika kila jambo na kudumisha amani ya Taifa letu. Hapo ndipo ahadi na mipango yetu itatimia,” alihitimisha Waziri Mkuu Mteule.

No comments:

Post a Comment