
OWM-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Mhe. Reuben Kwagilwa, amewataka watumishi wa Idara ya Elimu katika Ofisi hiyo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu watendaji walio chini yao ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Akizungumza na wasimamizi wa Idara ya Elimu katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Jjijini Dodoma leo Novemba 21, 2025 Mhe. Kwagilwa amesema utekelezaji wa majukumu kwa weledi utasaidia kufikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuleta tabasamu kwa Watanzania kupitia maboresho ya sekta mbalimbali ikiwemo elimu.
“Mheshimiwa Rais anatamani wizara hii ambayo inagusa wananchi moja kwa moja inapeleka tabasamu kwa watanzania hao lakini twendeni tukafanye udhibiti na tukatimize majukumu yetu kwa weledi kama ambavyo mmekuwa mkifanya siku zote.” Amesema
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Atupele Mwambene, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI inaendelea kushirikiana na Wizara mbalimbali kama vile Wizara ya Elimu, Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.
Mwambene aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa hususani katika maeneo yenye changamoto kwani dhamira ya Serikali ni kuona kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora, salama na yenye usawa.




No comments:
Post a Comment