MAVUNDE AKABIDHI VIFAA KUBORESHA ELIMU, AONDOA MZIGO WA MICHANGO YA MITIHANI MTUMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 15, 2025

MAVUNDE AKABIDHI VIFAA KUBORESHA ELIMU, AONDOA MZIGO WA MICHANGO YA MITIHANI MTUMBA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Mhe. Anthony Mavunde, amekabidhi vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa shule za msingi na sekondari ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza mzigo wa michango ya mitihani ambayo wazazi walikuwa wakitozwa kila Jumamosi.

Katika hafla hiyo, Mhe. Mavunde amekabidhi mashine za fotokopi kwa kata 20, kompyuta mpakato 20 kwa waratibu elimu kata na kompyuta mpakato 90 kwa walimu wakuu na wakuu wa shule za Serikali katika Jimbo la Mtumba.

Amesema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika maandalizi ya mitihani, ufundishaji na usimamizi wa elimu, hatua itakayopunguza mzigo kwa wazazi na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Aidha, amewataka walimu kuimarisha umoja na ushirikiano ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika baadhi ya masomo, sambamba na kuongeza kasi ya kuinua kiwango cha elimu jimboni humo.

Mbunge huyo ameahidi kuendelea kuboresha mazingira ya elimu, huku akitangaza mpango wa kuanzisha SACCOS ya walimu wa Jimbo la Mtumba, ambayo atawekea shilingi milioni 20 kama mtaji wa kuanzia ili kuwawezesha walimu kiuchumi.

“Tutashirikiana na Serikali kujenga miundombinu bora na kutatua changamoto katika sekta ya elimu, kwa kuwa elimu ndiyo kipaumbele chetu kikubwa,” alisema Mavunde.

Vilevile, ameahidi kuendeleza vipaji vya watoto kupitia Shindano la Mavunde na kuanzisha mashindano mengine ndani ya jimbo hilo ili kukuza uwezo wa wanafunzi katika nyanja mbalimbali.

Akizungumzia mchango wake kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Mhe. Mavunde alisema tayari ameanzisha Mavunde Foundation, yenye lengo la kuwawezesha watoto kupata elimu na kujikwamua kimaisha.

Ametoa wito kwa walimu wakuu na waratibu elimu kata kuhakikisha vifaa walivyokabidhiwa vinatunzwa na kutumiwa ipasavyo ili kutatua changamoto za elimu na kupunguza gharama kwa wazazi.









No comments:

Post a Comment