
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Serikali imesema itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na kampuni za uchimbaji madini nchini, ili kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na migodi wananufaika moja kwa moja na shughuli za uchimbaji madini.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, alisema hayo hivi karibuni alipokagua utekelezaji wa miradi ya CSR inayofanywa na kampuni za uchimbaji madini katika mkoa huo, akibainisha kuwa miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya umeme.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi. Ndiyo maana tunasisitiza kampuni zote za uchimbaji, zikiwemo zinazomilikiwa na wachimbaji wadogo, kutekeleza wajibu wao wa kijamii kupitia miradi ya CSR ili jamii inayoishi jirani na migodi inufaike moja kwa moja na rasilimali hizo,” alisema Makolobela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya EMJ Mining iliyopo eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Masanga Silanga, alisema kampuni hiyo inajihusisha na uchimbaji wa dhahabu kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka China, jambo lililoongeza ufanisi na teknolojia katika shughuli zao za uchimbaji.
Alisema kampuni hiyo huzalisha wastani wa kilo 10 za dhahabu kwa mwezi endapo kuna upatikanaji mzuri wa mwamba wenye madini (mbale), ingawa wakati mwingine hukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mwamba kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na mishororo midogo ya dhahabu (narrow vein).
Silanga alibainisha kuwa kampuni yake imetekeleza miradi kadhaa ya CSR ikiwemo kutoa madawati 50 na matofali 2,000 kwa Shule ya Msingi Dutwa, mashine za kuchapisha (printer) na nakala (photocopy) kwa taasisi za elimu, pamoja na mchango wa matofali 2,000 kwa Hospitali ya Nguno.
“Tayari tumewekeza zaidi ya Dola 50,000 katika miradi ya CSR, ikiwemo mradi wa kuvuta umeme kutoka Dutwa hadi vijiji vya jirani ambavyo awali havikuwa na huduma ya umeme,” alisema Silanga.
Naye Meneja wa Mgodi huo, Noah Wang, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni upungufu wa mwamba wenye madini (mbale), hali inayosababisha baadhi ya mitambo kusimama na kupunguza uzalishaji.
“Mitambo yetu ina uwezo wa kuchakata hadi tani 500 za mwamba kwa siku, lakini kwa sasa hatupati kiwango hicho, jambo linalolazimisha baadhi ya mitambo kuzimwa mara kwa mara. Kwa sasa shaft moja pekee ndiyo inaendelea na kazi, hivyo uzalishaji umeshuka kwa kiasi kikubwa,” alisema Wang.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeajiri jumla ya wafanyakazi 48, wakiwemo 30 wazawa na 18 raia wa China, wanaofanya kazi kwa mfumo wa kupokezana (shift system).





No comments:
Post a Comment