
Na Sixmund Begashe, Arusha
Zoezi la ukusanyaji wa taarifa na takwimu kwa ajili ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2022/2023 – 2025/2026, limeonekana kuwa chachu ya maboresho zaidi ya shughuli zinazotekelezwa na taasisi za wizara hiyo pamoja na jumuiya za kijamii nchini.
Hayo yamebainika jijini Arusha katika zoezi hilo linaloongozwa na Mtaalamu Mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. Francis Mwaijande, likihusisha taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya maliasili na utalii.
Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi, Dkt. Joseph Makero, amesema zoezi hilo litasaidia chuo hicho kujipanga kikamilifu katika uundaji na utekelezaji wa mikakati inayochochea maendeleo endelevu ya mazao ya misitu.
“Zoezi hili lenye lengo la kuandaa Mpango Mkakati mpya wa Wizara (2026/2031) limetupa elimu ya namna bora ya kuandaa na kutathmini mikakati ili iweze kutumika katika kupanga hatua nyingine za maendeleo kwa miaka ijayo,” amesema Dkt. Makero.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Lembris Luipuko, amepongeza utaratibu wa wizara kufanya zoezi hilo kwa ushirikiano na wadau ambalo linaibua matumaini ya neema zaidi kwa wanachama wao na kwamba matokeo ya tathmini hiyo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya sekta ya utalii, uboreshaji wa miundombinu na vivutio vya utalii nchini.
Zoezi hilo pia limehusisha taasisi mbalimbali zikiwamo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) pamoja na Chama cha Waendesha Utalii Tanzania (TATO).






No comments:
Post a Comment