Akizungumza leo tarehe 10 Novemba 2025, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya CCM 2025–2030, pamoja na ahadi za kampeni na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nane.
Amesema Serikali itaendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuimarisha sekta za uzalishaji, uwekezaji, sekta binafsi, na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwa na lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7 hadi 10 kwa mwaka, kudhibiti mfumko wa bei chini ya asilimia 5, kuzalisha ajira mpya 350,000, na kuongeza kipato cha mwananchi hadi Dola 1,880 kufikia mwaka 2030.
Aidha, Serikali itatekeleza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, bandari za abiria Mpigaduri, Kizimkazi, Shumba na Wete, pamoja na boti mbili za kisasa za mwendo kasi zitakazohudumia safari kati ya Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam.
Katika sekta ya afya, Serikali itajenga hospitali nne za mikoa, kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Saratani Binguni, na kuboresha Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Katika elimu, Serikali itajenga madarasa mapya 2,000, shule tatu za sekondari za wasichana kwa kila mkoa, chuo cha kisasa cha ualimu, na kuajiri walimu 7,691.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kuongeza mafunzo, maslahi na nidhamu ya kazi, huku taasisi za ZAECA na CAG zikiimarisha mifumo ya udhibiti wa rushwa na matumizi sahihi ya fedha za umma.
Vilevile, Serikali itajenga vituo viwili vya utamaduni Unguja na Pemba, kuendeleza michezo, na kukamilisha maandalizi ya AFCON 2027.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar linatarajiwa kuanza rasmi shughuli zake tarehe 11 Februari, 2026.







No comments:
Post a Comment