
Na Okuly Julius,OKULY BLOG, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Uchunguzi ya yaliyotokea Oktoba 29 kuchunguza kwa kina chanzo, viongozi, na misukumo yote iliyopelekea vurugu zilizosababisha taharuki nchini, akisisitiza kuwa taifa haliwezi kuruhusu hali kama hiyo kujirudia.
Akizindua tume hiyo jijini Dodoma, Rais Samia alisema hatua hiyo inalenga kupata ukweli kamili wa kilichojiri, ili serikali na wadau wengine waweze kuchukua hatua sahihi na kurejesha imani ya wananchi kwa mifumo ya kisiasa na kisheria.
“Kwa ufupi nataka kusema yafuatayo, kwanza tunatarajia Tume ituangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile ni nini. Kiini cha tatizo ni nini? Na wakati inatokea kadhia ile vijana waliingizwa barabarani kudai haki — tunataka kujua haki gani ambayo vijana hawa wameikosa hadi wakaingia barabarani kwa umoja wao. Lengo lao lilikuwa nini?” alisema Rais Samia.
Ameitaka Tume hiyo kuchunguza pia matamshi na mienendo ya baadhi ya vyama vya upinzani wakati wa tukio hilo, akisema kuwa kauli za uchochezi zinaweza kuwa zimechangia kuharibu hali ya usalama.
“Tuangalie matamshi ya vyama vya upinzani. Walisema lazima kiwake, hapakaliki, lazima aondoke. Ni kitu gani kilichowafanya waseme hivyo? Na uhusiano wao na Tume ya Uchaguzi ulikuwaje katika kipindi hicho?” alihoji.
Rais Samia alibainisha kuwa pamoja na uzito wa majukumu, tume hiyo imeundwa kwa kufuata sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 2023, na imepewa hadidu za rejea mahsusi zitakazowaongoza katika kazi yao.
“Tumewapa mzigo mzito, lakini kwa sifa zenu mtaweza. Nimetaka tume ya ndani ianze kazi kabla hatujawaita wengine kutoka nje. Wakija, watakutana na tume wenzao ambao tayari wameanza.”
Kuhusu madai kuwa baadhi ya vijana waliingia mitaani kutokana na kulipwa fedha, Rais Samia ameitaka tume kuchunguza kwa kina ushiriki wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), ya ndani na nje, ambayo yanaweza kuwa yalihusika kuyachochea.
“Naambiwa kwamba vijana walilipwa fedha kwanza ndipo wakaingia barabarani. Fedha zilitoka wapi? Tuangalie mchango wa NGO zetu za ndani na nje kwenye hilo,” alisisitiza.
Aidha, Rais Samia ametaka tume kuchunguza ikiwa kulikuwa na njia nyingine za kutatua changamoto kati ya vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi, Msajili wa vyama na serikali, badala ya kufikia hatua ya vurugu, uchomaji na vifo.
“Je hakukuwa na njia nyingine ya kurekebisha kasoro zilizokuwepo? Kwa nini njia ikawa kuingia barabarani na kuchafua nchi?”
Amesema tume pia itahitaji kuchunguza namna vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoshughulikia vurugu hizo, ili kubaini kama hatua zilizochukuliwa zilikuwa sahihi na zimesaidia kudhibiti madhara.
“Kilichokuwa kinaimbwa ni kwamba kama Madagascar, ndivyo kitakavyokuwa hapa. Sasa tuangalie njia zilizotumika kukabiliana na vurugu hizo,” aliongeza.
Rais Samia aliihimiza tume kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na dhamira ya kulinda maslahi mapana ya nchi, akisema Watanzania wanahitaji majibu sahihi kuhusu kilichotokea na hatua za mbele katika kulinda amani ya taifa.





No comments:
Post a Comment