VICOBA VISIVYOSAJILIWA MATATANI - BoT - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 20, 2025

VICOBA VISIVYOSAJILIWA MATATANI - BoT


Meneja Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha (BoT), Dickson Gama, akiwasilisha mada katika semina kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na Benki hiyo.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wadau wa Vikundi vya huduma ndogo za fedha vya Kijamii (VICOBA) kuchukua hatua za haraka kurasimisha vikundi vyao, ikieleza kuwa kufanya hivyo kutaimarisha usalama wa fedha, kuongeza uwazi na kujenga imani ya wanachama.

Hatua hii imekuja wakati ambapo Vikundi hivyo (VICOBA) vinaendelea kuwa nguzo muhimu kwa wananchi wanaojitafuta kiuchumi, hususan wanawake na vijana wanaotegemea akiba ndogo ndogo na mikopo midogo kujenga biashara na kuboresha maisha ya kaya.

Meneja Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha (BoT), Dickson Gama, ameeleza hayo leo November 20 ,2025 Jijini Dodoma kwenye semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Benki hiyo na kueleza kuwa licha ya mchango mkubwa, bado vikundi vingi havijarasimishwa, jambo linalowafanya wanachama wengi kukosa ulinzi wa kisheria pale panapojitokeza migogoro au matumizi mabaya ya fedha.

"Adhabu za Kukiuka Kanuni – Huduma Ndogo za Fedha Daraja la Nne ni Faini kati ya Shilingi milioni 1 hadi Shilingi milioni 10 Kifungo au kisichopungua miezi 3 na kisichozidi miaka 2, au vyote kwa pamoja

Amesema pamoja na VICOBA kuwa chanzo kikuu cha mitaji kwa wananchi wa kipato cha chini, changamoto za usimamizi zisizoshughulikiwa zimekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa sekta hiyo.

Amezitaja changamoto kubwa zinayojitokeza kabla ya vikundi kusajiliwa kuwa ni ukosefu wa uwazi kwa baadhi ya viongozi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa zisizokidhi viwango au kufanya maamuzi bila kuwashirikisha wanachama.

Amesema Matendo hayo yamekuwa chanzo cha migogoro, malalamiko ya upendeleo katika utoaji mikopo na matumizi yasiyoeleweka ya fedha hali inayowakatisha tamaa wananchi wanaojaribu kujikwamua kimaisha kupitia mfumo wa VICOBA.

BoT pia imeeleza kuwa tatizo la kutotendewa haki kwa wanachama na ukosefu wa takwimu sahihi za sekta ya huduma ndogo za fedha limekuwa likikwamisha tathmini na upangaji wa mipango ya maendeleo ya vikundi.

Gama amesema uhaba wa taarifa unaendelea kuzuia usimamizi madhubuti kutoka kwa wadhibiti pamoja na Serikali za mitaa, hivyo kuathiri usalama wa fedha ambazo zinategemewa na familia nyingi kujikwamua na umaskini.

Ili kuimarisha mfumo huu, Serikali kupitia TAMISEMI imepewa jukumu kubwa kusimamia mchakato wa urasimishaji kwa kupokea na kuchakata maombi kupitia mfumo wa WEZESHA PORTAL, kutunza rejista ya kitaifa ya vikundi vilivyosajiliwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.

Hatua hizi zimekusudiwa kuhakikisha viongozi wanazingatia uadilifu, ulinzi wa wanachama na matumizi sahihi ya fedha za vikundi.

Kwa mujibu wa kanuni za uanzishwaji wa kikundi kipya unapaswa kuhusisha wanachama 10 hadi 50, mkutano wa awali wa kuchagua kamati ya muda na mkutano wa uanzishaji utakaofanyika chini ya afisa aliyeidhinishwa.

Taratibu hizi zinalenga kuhakikisha kuwa vikundi vinajengwa katika msingi imara wa uongozi, uwajibikaji na weledi kabla ya kutuma maombi ya usajili Benki Kuu au kwa mamlaka kasimishwa.

BoT inaeleza kuwa maombi ya usajili yanapaswa kuambatana na mihtasari ya mikutano, katiba ya kikundi, orodha ya wanachama, majina ya viongozi na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.

Maombi hayo huchakatwa ndani ya siku 14 na yanaweza kukataliwa endapo kikundi hakijakidhi vigezo vilivyowekwa, hadi kitakaporekebisha kasoro zote.

Baada ya kupokea usajili, kikundi kinatakiwa kuanza shughuli ndani ya miezi mitatu na kuzingatia masharti kama kuwa na ofisi rasmi, kufungua akaunti ya benki, kutunza rekodi sahihi za fedha na kuwasilisha taarifa za robo mwaka kwa mamlaka husika.

Ameeleza kuwa BoT na TAMISEMI pia wana mamlaka ya kufanya ukaguzi wa ghafla ili kulinda maslahi ya wanachama na kuzuia upotevu wa fedha zinazotegemewa na kaya nyingi.

Licha ya hayo amefafanua kuwa kutokana na changamoto za utunzaji kumbukumbu na usalama mdogo wa fedha, BoT imeeleza kuwa baadhi ya vikundi vinaanza kuhamia kwenye mifumo ya kidijitali kuongeza uwazi, ufuatiliaji na usimamiaji bora wa fedha.

Amesema vikundi vinavyokiuka kanuni vinaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kufutiwa usajili, kusimamishwa viongozi au kutozwa faini kati ya shilingi milioni moja hadi milioni kumi—hatua zinazolenga kulinda sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa kaya.

No comments:

Post a Comment