WADAU WA USIMAMIZI WA MAAFA WAKUTANA KUJADILI RASIMU YA MPANGO WA TAIFA WA DHARURA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 14, 2025

WADAU WA USIMAMIZI WA MAAFA WAKUTANA KUJADILI RASIMU YA MPANGO WA TAIFA WA DHARURA


Na Mwandishi Wetu- Dodoma


Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amewataka washiriki wa Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa kushiriki kikamilifu kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa kukabiliana na ukame, mafuriko na majanga mengine ili kuwa na mpango thabiti wa kuwezesha Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki za kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali kutokana na maafa yanayoweza kusababishwa na mwelekeo wa mvua za msimu.

Brigedia Jenerali Ndagala ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa leo tarehe 14 Novemba,2025 Jijini Dodoma.

“Kama mtakumbuka tarehe 17 Oktoba, 2025 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2025 hadi Aprili 2026, kufuatia utabiri huo, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu imeandaa Rasimu ya Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Ukame, Mafuriko na Majanga mengine”

“Rasimu hii itawasilishwa katika jukwaa hili la wadau wa Usimamizi wa mafaa kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni kwa kuzingatia utabiri wa msimu uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania” ameeleza Brigedia Jenerali Ndagala.

Aidha, amebainisha kuwa, jukwaa hilo ni muhimu ili kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya maandalizi ya msimu, hivyo, kuwataka Wadau hao kushiriki kikamilifu na kutoa maoni huku wakijielekeza kwenye athari tarajiwa na hatua zitakazochukuliwa.

Vilevile, Brigedia Jenerali Ndagala ameongeza kuwa pamoja na Rasimu ya Mpango wa dharura ulioandaliwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa miongozo ya Uanzishaji na Uendeshaji wa Vituo vya Operesheni za dharura na Timu za Kukabiliana na dharua ngazi za Mikoa ambayo pia itawasilishwa kwa ajili ya kupata maoni.

No comments:

Post a Comment