Ifakara, Kilombero
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Wakili Dunstan Kyobya, leo Jumamosi, Desemba 20, 2025, amekutana na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Ifakara kujadili masuala muhimu yanayohusu ustawi wa soko na shughuli zao za kibiashara.
Katika kikao hicho, Mhe. Kyobya amezungumzia masuala ya usafi wa soko, ulinzi na usalama, pamoja na mpango wa ujenzi wa soko jipya la kisasa. Aidha, amesikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na kusisitiza umuhimu wa wao kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Bi. Pilly Kitwana, amewahimiza wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa haraka, hatua itakayowawezesha kuendesha biashara zao katika mazingira safi, salama na yenye tija.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya na Halmashauri, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya uongozi na wafanyabiashara kwa maendeleo ya pamoja.









No comments:
Post a Comment