
Na Beatus Maganja, Dar es Salaam
TAMASHA la Funga Mwaka Kijanja Talii Msimu wa Pili linaloendelea katika viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam limeelezwa kuwa fursa muhimu kwa wakazi wa jiji hilo na Watanzania kwa ujumla kufanya utalii wa ndani kwa kushuhudia vivutio mbalimbali vya wanyama pori.
Tamasha hili lililoanza Disemba 2025 na kutazamiwa kufikia tamati Januari 05, 2026 ni sehemu ya kampeni kubwa ya kitaifa ya kuhamasisha utalii katika kipindi cha sikukuu na kufunga mwaka likiwa limeandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii Kupitia Bodi ya Utalii Tanzania.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea tamasha hilo mapema leo Disemba 24, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo ili kuweza kupata elimu ya namna ya kuwekeza katika sekta ya utalii nchini, namna ya kushiriki katika biashara ya nyara na kupata kitoweo cha nyamapori kwa njia halali sambamba na kujionea wanyamapori hai wa aina mbalimbali wakiwemo tembo na ngiri maarufu "Kasongo yeye"

"Tunawaomba wananchi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani waje viwanja vya SabaSaba Kilwa"Road" kujionea wanyamapori hai, mimi mwenyewe nimejionea Simba, duma, tembo, "Kasongo" (ngiri) pia yupo hapa" alisema Dkt. Abbas
Aidha Katibu Mkuu huyo amesema sekta ya utalii nchini iko imara, haijatikisika na inaendelea kuonesha ukuaji mkubwa licha ya changamoto mbalimbali zilizoikumba dunia na nchi yetu huku akibainisha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024 na kusisitiza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kufanya vizuri katika eneo hilo.
"Watalii wameongezeka Tanzania kwa asilimia 9 kati ya mwezi Januari mpaka mwezi Novemba 2025. Kwahiyo kitaifa tunalo ongezeko la watalii laki moja na sabini na tatu (173,000) ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana" alisema Dkt. Abbas
"Hata kwenye taasisi yetu ya TAWA, wanafanya vizuri sana, utalii unafanya vizuri. Kwa takwimu za TAWA watalii wameongezeka kwa asilimia takribani 18 wa kutoka nje ya nchi na wale wa ndani wameongezeka kwa asilimia 40" aliongeza Dkt. Abbas
Dkt. Abbas ameongeza kuwa ongezeko hilo linatokana na jitihada za serikali katika kutangaza utalii, kuimarisha miundombinu na kuhakikisha usalama katika hifadhi zote nchini, huku watalii wa ndani na wa nje wakiendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mlage Yusuf Kabange amesema lengo la kuanzisha tamasha hilo ni kuitikia maombi ya wananchi ya kutaka kupata wasaa mzuri zaidi wa kuona wanyamapori, maombi yaliyokuwa yakitolewa na wananchi katika kipindi cha maonesho ya biashara ya Kimataifa.
"Wakati tunafanya maonesho ya SabaSaba hapa, baadhi ya wananchi walileta maombi kwamba muda wa kuona wanyamapori hautoshi, sasa tukaona tuje na mikakati tofauti mkamati mmojawapo ni huu wa kuleta wanyama hawa wakati wa kipindi cha likizo ambapo wanafunzi watakuwa na nafasi ya kutosha na wazazi wao kuwasindikiza kuja kuona wanyamapori hawa" alisema Kabange
"Sasa ni kama tumehamisha mbuga kwa kuitoa porini na kuileta Dar es Salaam, kwakuwa tumeongeza wanyama ambao hawakuwepo katika maonesho mbalimbali yaliyopita ambao wananchi walihitaji wawepo kama vile tembo, ngiri na aina nyingine ya swala" aliongeza Kamishna Kabange









No comments:
Post a Comment