TUME YA UTUMISHI WA UMMA YASIKILIZA RUFANI 88, YATOA ONYO KWA WATUMISHI NA WAAJIRI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 23, 2025

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YASIKILIZA RUFANI 88, YATOA ONYO KWA WATUMISHI NA WAAJIRI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma


Tume ya Utumishi wa Umma imesikiliza na kutoa maamuzi juu ya rufaa na malalamiko 88 ya watumishi wa umma katika Mkutano wake wa pili kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 uliofanyika kuanzia Desemba 1 hadi 19, 2025, katika Manispaa ya Morogoro.

Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Mst.) Hamisa H. Kalombola, ulilenga kupokea, kusikiliza na kujadili rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume iliyotolewa leo Desemba 23, 2025 jijini Dodoma na Kaimu Katibu wa Tume hiyo, John Mbisso, jumla ya rufaa 63 na malalamiko 25 zilisikilizwa na kutolewa maamuzi.

Akizungumza kuhusu rufaa hizo, Mbisso amesema zilihusisha makosa mbalimbali ikiwemo utoro kazini, wizi wa mali za umma na rushwa, kughushi vyeti, kutoa taarifa za uongo, kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma, uzembe uliosababisha hasara kwa Serikali pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo.

Kwa upande wa malalamiko, amesema watumishi walilalamikia kutolipwa stahili zao ikiwemo mishahara, posho na mafao ya kisheria, kuondolewa kazini kinyume cha sheria pamoja na kusitishiwa ajira bila kufuata taratibu zilizowekwa.

Mbisso ameongeza kuwa katika mkutano huo, Tume iliita mbele yake Mamlaka za Nidhamu tano kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa maagizo ya awali ya Tume.

Aidha, Tume ilifanya ziara za kikazi katika taasisi tano za Serikali zilizopo Manispaa ya Morogoro ambazo ni Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).

Kupitia ziara hizo, Tume ilitoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi wa rasilimali watu. Vilevile, watumishi wa umma walielimishwa kuhusu haki na wajibu wao wanapotekeleza majukumu yao.

Mbisso amesema Tume itaendelea kusimamia haki, usawa na uwajibikaji katika Utumishi wa Umma kwa kuhakikisha rufaa na malalamiko ya watumishi yanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kwa haki.

Aidha, amewahimiza watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi na sheria wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka hatua za kinidhamu, huku akizitaka mamlaka za ajira na nidhamu kushughulikia masuala ya kiutumishi kwa haki na kwa kuzingatia misingi ya kisheria.

No comments:

Post a Comment