GCLA YAONYA VIWANDA VINAVYOKIUKA SHERIA ZA USIMAMIZI WA KEMIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 2, 2025

GCLA YAONYA VIWANDA VINAVYOKIUKA SHERIA ZA USIMAMIZI WA KEMIKALI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewataka wamiliki wa viwanda vinavyotumia kemikali kuhakikisha wanazingatia kikamilifu sheria za usimamizi wa kemikali pamoja na miongozo ya usalama mahali pa kazi ili kulinda afya za wafanyakazi na mazingira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao cha kujadili udhibiti wa sumu ya risasi na madhara yake, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira wa GCLA, Dkt. Shimo Peter, amesema uchunguzi umebainisha kuwepo kwa uzembe katika baadhi ya viwanda ikiwemo kutotumia vifaa sahihi vya kujikinga na kemikali hatarishi.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya viwanda vitakavyokiuka sheria hizo, kwani uzembe huo unaweka hatarini maisha ya wafanyakazi na kuathiri mazingira.

Akifafanua kuhusu sumu ya risasi, Dkt. Shimo amesema sumu hiyo hutokana na mkusanyiko wa risasi mwilini kwa kipindi cha miezi au miaka, na hata kiwango kidogo kinaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya.

Ameeleza pia kuwa Dunia huadhimisha Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Sumu ya Risasi (ILPPW) kila mwaka katika wiki ya tatu ya Oktoba. Mwaka 2025 maadhimisho hayo yalipangwa kufanyika Oktoba 19–25, kipindi ambacho Tanzania ilikuwa ikifanya uchaguzi mkuu.

Ujumbe wa ILPPW 2025 ulihusu kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mfiduo wa risasi, ukiwa na kaulimbiu: “Hakuna kiwango salama: Chukua hatua sasa kumaliza mfiduo wa risasi.”

No comments:

Post a Comment