GEREZA LA KIBONDO LABUNI MKAA MBADALA KUTEKELEZA AGIZO LA SERIKALI LA NISHATI SAFI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 15, 2025

GEREZA LA KIBONDO LABUNI MKAA MBADALA KUTEKELEZA AGIZO LA SERIKALI LA NISHATI SAFI



Jeshi la Magereza wilayani Kibondo mkoani Kigoma limeanza kutumia mkaa mbadala unaotokana na mchanganyiko wa maranda ya miti na udongo unaozalishwa ndani ya Gereza la Kibondo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hayo yamebainika wakati wataalamu kutoka Wizara ya Nishati walipotembelea gereza hilo kwa lengo la kukagua na kujionea utekelezaji mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma nchini.

Mkuu wa Gereza la Kibondo, Bw. Peter Shabani, amesema gereza hilo lilichukulia agizo la Serikali kama fursa ya ubunifu na kujitegemea kwa kutumia rasilimali zilizopo hatua ambayo inalenga kulinda afya, mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati

“Baada ya agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia, sisi kama Gereza la Kibondo tulilichukulia kama fursa. Kupitia wataalamu tulionao na kwa kushirikiana na wafungwa, tuliweza kubuni nishati yetu wenyewe kwa kutumia malighafi tulizonazo ili kupunguza gharama za kuagiza nishati kutoka nje." Amesema Bw. Shabani

Ameeleza kuwa mkaa huo mbadala umebuniwa na wafungwa waliopo gerezani hapo kama sehemu ya programu za urekebishaji tabia akibainisha kuwa kwa sasa nishati hiyo inatumika kwa matumizi ya ndani pekee kutokana na uhaba wa vifaa vya kisasa vya uzalishaji.


Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw. Masumbuko Noha, amepongeza hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na viwango vya TBS endapo gereza hilo litaanza uzalishaji wa nishati hiyo kwa matumizi ya kibiashara.

“Ubunifu huu una tija kubwa, lakini ni muhimu kuhakikisha bidhaa hiyo inakidhi viwango vya ubora na usalama kabla ya kuanza kuuzwa kwa matumizi ya jamii,” amesema Bw. Noha

Naye mtaalam kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Omary Khalifa, amesema ubunifu huo ni mfano mzuri wa utekelezaji wa sera ya nishati nchini, akilishauri Jeshi la Magereza Kibondo kuendeleza wazo hilo ili liwe fursa ya kiuchumi na chachu kwa taasisi nyingine.

“Hatua hii inaweza kuwa dira kwa taasisi nyingine nchini kuiga na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, sambamba na kulinda mazingira na afya za wananchi,” amesema Bw. Khalifa





No comments:

Post a Comment