Na Meleka Kulwa – Dodoma
Wananchi zaidi ya 6,800 wa kata ya Bahi na Kata ya Makutupora Jijini Dodoma wanatarajiwa kunufaika na miradi ya maji safi na salama inayotekelezwa na Shirika la Habitat for Humanity Tanzania katika kata ya bahi wilaya ya bahi na mtaa wa Mchemwa uliopo Jimbo la Mtumba, Kata ya Makutupora.
Mkurugenzi wa Miradi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, amezungumza na wazazi, wakuu wa Shule za Msingi Mchemwa na Mbande, viongozi wa serikali za mitaa pamoja na maafisa mbalimbali Desemba 12, 2025 Jijini Dodoma, kuhusu utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kupitia Mradi wa WASH for Food Security, unaolenga kuondoa adha ya ukosefu wa maji iliyodumu kwa miaka mingi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa mradi huo, Habitat for Humanity Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii zitakazoboresha maisha yao, huku akibainisha kuwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Aidha amebainisha kuwa maji ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa jamii, huku akifafanua kuwa dira ya shirika hilo ni kuwa na Taifa ambalo kila mtu anakuwa na mahali pa kuishi.
Aidha amebainisha kuwa mradi huo utagharimu shilingi milioni 300 za Kitanzania na utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu.
Amesema kuwa mradi huo utakapokamilika utapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mitaa ya Azimio, Mchemwa na Mbande, huku akibainisha kuwa nusu ya wakazi wa maeneo hayo wanakumbwa na changamoto ya ukosefu wa maji.
Aidha amebainisha kuwa kupitia mradi huo, Habitat for Humanity Tanzania inalenga kupunguza changamoto ya usalama wa chakula kwa wakazi wa maeneo hayo, akifafanua kuwa Jiji la Dodoma lina uhaba wa mvua na kupitia mradi huo wananchi wataweza kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
Amesema kuwa shirika hilo litawahamasisha na kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha umwagiliaji cha mazao ya biashara na matumizi ya nyumbani, huku akibainisha kuwa kupitia mradi huo wananchi watakuwa na uhakika wa kulima na kuvuna.
Aidha amebainisha kuwa miradi mingi ya maji hushindwa kuendelea kutokana na baadhi ya wananchi kushindwa kulipia gharama za umeme, hali inayosababisha miradi hiyo kushindwa kuendeshwa kwa ufanisi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
Amesema kuwa mradi wa maji utakaotekelezwa katika mtaa wa Mchemwa utatumia vyanzo viwili vya nishati ambavyo ni umeme na nishati ya jua, huku akibainisha kuwa matumizi ya nishati ya jua yatasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shule ya Msingi Mchemwa amesema kuwa mradi huo ni neema kubwa kwa wakazi wa mitaa ya Azimio, Mchemwa na Mbande. Aidha ametoa shukran kwa Habitat for Humanity Tanzania pamoja na wadau wote walioshiriki kushauri na kuwa mradi huo utekelezwe katika mtaa wa Mchemwa na maeneo jirani.






No comments:
Post a Comment