JMAT YALAANI MACHAFUKO YA OKTOBA 29, YAISHAURI SERIKALI NA JAMII KUANZA SAFARI YA MARIDHIANO MAPYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, December 3, 2025

JMAT YALAANI MACHAFUKO YA OKTOBA 29, YAISHAURI SERIKALI NA JAMII KUANZA SAFARI YA MARIDHIANO MAPYA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imetoa tamko rasmi likiitaka Serikali, viongozi wa dini, vijana na jamii kwa ujumla kuanza safari mpya ya maridhiano baada ya kadhia ya Oktoba 29, 2025 iliyoacha majeraha makubwa nchini wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Machafuko hayo, yaliyosababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi pamoja na taharuki ya kitaifa, yametajwa na JMAT kuwa ni “jeraha la kitaifa linalohitaji uponyaji wa pamoja, hekima na majadiliano ya kina.”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Alhad Mussa Salum, alisema jumuiya hiyo imefanya uchambuzi wa kina kuhusu matukio hayo na kubaini sababu kadhaa za kuzuka kwa machafuko, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ushawishi wa baadhi ya wanaharakati, kukata tamaa kwa vijana, hisia za udini na misimamo mikali ya kisiasa.
“Taifa lina majeraha ya ndani” – JMAT

Sheikh Salum alisema athari za machafuko hayo zimejidhihirisha sio tu kwenye uharibifu wa mali, bali pia katika afya ya akili, hisia na utengamano wa kijamii.

“Kadhia hii imeacha chuki, hofu na mgawanyiko. Wapo waliopoteza wapendwa, wengine mali, na wengi amani ya moyo. Haya yote yanahitaji maridhiano ya kweli,” alisema.

Jumuiya hiyo ilitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwataka Watanzania kuwaombea marehemu, kuwasaidia majeruhi na kuunga mkono juhudi za kurejesha utulivu bila kujali itikadi zao.

Katika tamko hilo, JMAT ilibainisha kuwa idadi kubwa ya vijana walijihusisha na maandamano kutokana na kushawishiwa kupitia mitandao ya kijamii, changamoto za ajira na kukata tamaa juu ya mustakabali wa maisha yao.

“Tatizo la vijana si jazba; ni mfumo unaowatenga na kuwakatisha tamaa. Hali hiyo huwafanya kuwa rahisi kushawishiwa. Taifa linawajibika kuwasimamia na kuwajengea matumaini,” alisema Sheikh Salum.

JMAT imeishauri Serikali kufanya uchunguzi wa wazi, wa kina na wa haki kuhusu chanzo cha machafuko hayo ili taifa lipate majibu sahihi. Pia imependekeza kufanyika kwa mkutano wa kitaifa wa maridhiano utakaowakutanisha Serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa, wanaharakati na wawakilishi wa vijana.

“Hatutaweza kuponya taifa kwa kufunika makovu. Ni lazima tuketi, tuseme ukweli, tusameheane na kupanga mikakati ya kuizuia historia kujirudia,” alisema.

Katika jitihada za kuliponya taifa kiroho na kiakili, JMAT imependekeza kufanyika kwa maombi ya kitaifa kwa siku tatu, yakihusisha waumini wa dini zote katika mikoa yote nchini.

Mitandao ya kijamii yaonywa
Jumuiya hiyo imeitaka Serikali kuimarisha udhibiti wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ikisema imekuwa chanzo kikuu cha uchochezi, upotoshaji na kusambaa kwa taarifa za chuki.

JMAT imeipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua ilizochukua baada ya machafuko, ikiwemo kulinda amani, kuimarisha utulivu na kuhimiza umoja wa kitaifa.

Pia jumuiya imempongeza Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa juhudi zake katika kurejesha utulivu miongoni mwa jamii na viongozi wa dini.

Katika tamko lake, JMAT imewaonya viongozi wa dini wanaotoa matamko yenye kuchochea chuki, ubaguzi au migawanyiko, ikisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume na misingi ya dini zote.

Aidha, imewataka vijana kuacha kurudia makosa ya Oktoba 29, na badala yake kujikita katika ujenzi wa amani, kushiriki katika maendeleo na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali.

JMAT imewaonya Watanzania kutoshiriki maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Desemba 9, 2025, ikisema yanaweza kuathiri heshima ya taifa, kusababisha machafuko mapya na kuendeleza mgawanyiko.

Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa huu ni wakati wa kusameheana, kujenga upya, kuponya majeraha na kuanzisha mjadala mpya wa kitaifa wa umoja na utengamano.

“Tanzania tuliirithi ikiwa na amani. Tuilinde. Tukosee, tusahihishe, tusameheane. Hivyo ndivyo mataifa makubwa hujengwa,”




No comments:

Post a Comment