KILANGO AWAHAMASISHA VIJANA SAME MASHARIKI KUSHIRIKI MKUTANO WA WAZIRI WA MAENDELEO YA VIJANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 22, 2025

KILANGO AWAHAMASISHA VIJANA SAME MASHARIKI KUSHIRIKI MKUTANO WA WAZIRI WA MAENDELEO YA VIJANA



SAME. Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Anne Kilango, amewasihi vijana wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufanyika Leo 22 Desemba 2025, katika viwanja vya Stendi ya Mabasi Ndungu, kufuatia ujio wa Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka.

Akizungumza kuelekea siku hiyo, Kilango alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuunda Wizara ya Maendeleo ya Vijana, wizara ambayo amesema itakuwa na mchango mkubwa katika kushughulikia changamoto, mafanikio na kero zinazowakabili vijana nchini.

Kilango alisema kundi la vijana ndilo kubwa zaidi nchini likiwa na takribani asilimia 64 ya Watanzania wote, hali iliyomfanya aone umuhimu wa kuwakusanya vijana wa Jimbo la Same Mashariki ili wapate nafasi ya kumsikiliza Waziri wao na kushiriki moja kwa moja katika majadiliano yanayowahusu.

Aliongeza kuwa hotuba itakayowasilishwa na Waziri wa Maendeleo ya Vijana haitahusu tu vijana wa Same Mashariki bali itakuwa ni hotuba yenye mwelekeo wa kitaifa, itakayobeba sera, mipango na fursa mbalimbali zitakazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii.

Mbunge huyo aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kueleza changamoto zao, kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia serikali kuboresha sera na programu za maendeleo ya vijana, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya taifa.

No comments:

Post a Comment