
Angela Msimbira, OWM–TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Sospeter Mtwale, amewataka Wakuu wa Vitengo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa nchini kuwajibika katika usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango stahiki.
Bw. Mtwale ametoa wito huo leo Desemba 15, 2025, wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Vitengo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa, yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.
Amesema Serikali inasisitiza usimamizi mzuri wa miradi ili iwanufaishe wananchi, kwani imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa majengo ya utawala, nyumba za watumishi, vituo vya afya, madarasa, mabweni na maabara katika maeneo mbalimbali nchini.
Bw. Mtwale amesisitiza kuwa, kutokana na ukubwa wa uwekezaji huo, Wakuu wa Vitengo wanao wajibu wa kutembelea miradi mara kwa mara, kuifuatilia hatua kwa hatua na kusimamia utekelezaji wake kwa kuzingatia mikataba ya utekelezaji wake.
“Nyie ndiyo wataalam wa Serikali, hakikisheni miradi yote inatekelezwa kwa ubora unaostahili ili thamani ya fedha ionekane wazi kwa wananchi,” amesisitiza Bw. Mtwale.
Aidha, Bw. Mtwale amesema Serikali imeongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika muundo wa Mkoa ili kuimarisha usimamizi wa miradi na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
Pia amewataka Wakuu wa Vitengo kushirikiana kwa karibu na Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ili taarifa za utekelezaji wa miradi pamoja na utatuzi wa kero za wananchi ziwafikie wananchi kwa wakati.
Amehitimisha kwa kuwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili miradi ya maendeleo iwe chachu ya ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Tawala za Mikoa, Bw. Ibrahim Minja, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo kitaalamu na kuwakumbusha wajibu wao wa msingi katika utumishi wa umma.

No comments:
Post a Comment