Akizungumza leo wakati wa ibada ya kumuaga iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, jijini Dodoma, Rais amesema marehemu alikuwa mlezi wa wengi ndani ya Bunge na Serikali, akisimama imara kutetea haki, maendeleo na ustawi wa watu aliowaongoza.
Rais Samia ameeleza kuwa Jenista Mhagama alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana, na mfano wa uongozi uliotawaliwa na nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu.
Amesema kupitia ibada hiyo, amepata fursa ya kuyafahamu kwa undani maisha ya kiroho na kidini ya marehemu, tofauti na alivyozoea kumfahamu zaidi kupitia majukumu yake serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Marehemu Jenista alikuwa mwalimu kwa taaluma, na alitumia kipawa chake cha ualimu kulea viongozi wengi. Aliwahi kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM na Mwenyekiti wa Bunge," amesema huku akisisitiza;
Wabunge na mawaziri walimheshimu sana, na katika nafasi hizo ametoa mchango mkubwa kwa wabunge, chama na Baraza la Mawaziri," amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa marehemu alikuwa mtu pekee aliyewahi kuvaa kofia mbili kwa wakati mmoja, yaani Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na Mnadhimu wa Serikali Bungeni, na aliweza kuzibeba kwa ufanisi mkubwa.
Rais Samia amesema Jenista Mhagama alikuwa kiongozi asiye na mzaha katika kazi, lakini mcheshi, mtii kwa mamlaka, chama chake na wananchi wake, huku akiwa mnyenyekevu mbele za Mungu.
Amesema alipata fursa ya kufanya kazi chini ya Serikali yake katika nafasi mbalimbali ikiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora) pamoja na Waziri wa Afya.
"Nilimpa jina la 'kiraka' kwa sababu kila nilipomuweka, aliziba vizuri. Alikuwa kiongozi anayejali maslahi ya wengi bila ubaguzi na bila kujali changamoto," amesema Rais Samia.
Amesema kupitia sauti yake bungeni, vitendo vyake katika jamii na msimamo wake katika uongozi, marehemu ameacha kumbukumbu njema na ameandika hadithi nzuri ya maisha yake ya utumishi.
Rais Samia amewataka wabunge na mawaziri, hususan wale wapya, kufuata nyayo za marehemu kwa kudumisha mshikamano bila kujali tofauti za kisiasa, kufanya mijadala ya kistaarabu inayolinda heshima ya Bunge, na kutimiza wajibu wao kwa uadilifu.
"Safari ya uongozi wa Jenista haikuwa rahisi, lakini aliitendea kwa ujasiri, hekima na heshima. Leo tunapomuaga, tunabaki na kumbukumbu ya tabasamu lake. Tutamkosa sana, kwa sababu tumepoteza mtu muhimu sana kwa taifa letu," amesema.
Rais Samia ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu, Spika wa Bunge, wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Jimbo la Peramiho, akisema taifa lote lipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Ameomba Mwenyezi Mungu awape faraja, nguvu na amani.
"Mdogo wangu Jenista, umetimiza wajibu wako ipasavyo na umepigana vita vilivyokupasa. Mwenyezi Mungu akupe safari ya kheri na ailaze roho yako mahali pema peponi. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina." ameeleza.


No comments:
Post a Comment