
Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG DODOMA
SERIKALI imesema itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii hadi milioni nane ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoelekeza katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Imepanga kutatua Changamoto za kikodi na zisizo za kikodi zinazokwamisha ukuaji wa sekta ya utalii ili kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani wa sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, leo Jumatatu, Desemba 15, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhi Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards 2025) iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
Dkt. Kijaji amesema changamoto hizo endapo zipo ndani ya Sera na Sheria ya Utalii, zinapaswa kusimamiwa kikamilifu na Idara ya Utalii ili kuhakikisha hazikwamishi watalii kufika nchini wala kuathiri uwekezaji katika sekta hiyo.
Ameielekeza Idara ya Utalii kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na sheria hizo kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii ili kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa zaidi cha utalii duniani.
Akizungumza baada ya kupokea rasmi tuzo hizo, Dkt. Kijaji amesema mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada mahsusi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kupitia filamu ya Royal Tour iliyolitangaza Taifa kimataifa.
Ameeleza kuwa tuzo hizo, zilizotolewa katika hafla ya kimataifa iliyofanyika Desemba 6, 2025 nchini Bahrain, ni uthibitisho wa mafanikio ya Sekta ya Utalii na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kupitia Royal Tour, dunia imejionea kwa macho yake utajiri wa vivutio vyetu vya asili, malikale, utamaduni pamoja na fursa za uwekezaji wa utalii,” amesema.
Ameongeza kuwa jitihada hizo zimeimarisha taswira ya Tanzania kama nchi salama, yenye amani na vivutio vya kipekee, hali iliyopelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii, kuimarika kwa imani ya wawekezaji na ushindani mkubwa wa Tanzania katika soko la utalii duniani.
Dkt. Kijaji ameishukuru sekta binafsi kwa mchango wake katika mafanikio hayo na kuahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wa utalii.
Awali, akitoa maelezo kuhusu tuzo hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi alieleza kuwa Tanzania imeibuka mshindi wa tuzo tano (5) ambazo zinajumuisha tuzo ya nchi ya Tanzania, Taasisi za Serikali pamoja na wadau binafsi.
“Tanzania ilishinda tuzo hizi katika Hafla ya 32 ya “World Travel Awards 2025”, iliyofanyika tarehe 6 Desemba 2025 nchini Bahrain, ambapo Tanzania iliendelea kushikilia taji la Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari kwa mara ya tatu mfululizo. Pia, Hifadhi ya Taifa Serengeti ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora ya Taifa Duniani 2025, Kisiwa cha Zanzibar (Spice Islands) kiliibuka mshindi wa “World MICE Awards 2025 kama Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi.” Alieleza Dkt. Abbasi
Aidha, tuzo za wadau na makampuni binafsi zilikuwa ni pamoja na Serengeti Balloon Safaris ambayo ilitwaa tuzo ya Kampuni Bora ya Utalii wa wa Puto Duniani, na Jumaira Thanda Resort iliyopo Kisiwa cha Mafia iliyotangazwa mshindi katika kipengele cha Kisiwa Bora cha Mapumziko Duniani hali iliyothibitisha hadhi na ubora wa vivutio vya mapumziko na huduma za ukarimu nchini kwa viwango vya kimataifa.
Katika Tuzo za World Travel Awards 2025, Tanzania imeibuka kidedea kwa kushinda tuzo za World’s Leading National Park – Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, World’s Leading Balloon Ride Operator – Serengeti Balloon Safaris, World’s Leading Exclusive Private Island – Jumeirah Thanda Island pamoja na Africa’s Best Corporate Retreat Destination – Zanzibar.




No comments:
Post a Comment