‎WANAFUNZI 145 WENYE ULEMAVU WACHAGULIWA VETA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 23, 2025

‎WANAFUNZI 145 WENYE ULEMAVU WACHAGULIWA VETA



‎Na. Meleka Kulwa-Dodoma


‎Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imewachagua wanafunzi 145 wenye ulemavu na mahitaji maalum kujiunga na vyuo vya VETA kwa mwaka wa masomo 2026 hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha usawa na ujumuishi katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

‎Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 23, 2025, Makao Makuu ya VETA jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa jumla ya waombaji 195 wenye mahitaji maalum waliomba kujiunga na vyuo vya VETA, ambapo 145 tayari wamechaguliwa kujiunga na vyuo 53 vya VETA, huku waombaji wengine 50 wakiendelea kusubiri kupangiwa.

‎Adha amebainisha kuwa waombaji hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uoni hafifu, usikivu hafifu na ulemavu wa viungo, huku akibainisha kuwa serikali italipa ada za mafunzo kwa waombaji wote 195 kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya pili ili kuondoa vikwazo vya gharama.

‎Mbali na hayo CPA Kasore amesema kuwa mchakato wa uchaguzi wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026 umefanyika kwa kuzingatia miongozo na mifumo rasmi ya Serikali, ambapo zoezi hilo limekamilishwa kwa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETMIS).

‎Amebainisha kuwa kwa mwaka huu jumla ya waombaji 18,875 walichukua fomu za kuomba kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA, kati yao wanawake walikuwa 6,915 sawa na asilimia 37 na wanaume 11,960 sawa na asilimia 63.

‎Pia, CPA Kasore, amesema kuwa uchaguzi wa waombaji umezingatia vigezo mbalimbali ikiwemo kipaumbele kwa waombaji waliowahi kuomba awali, uwezo wa kila chuo kwa kila fani, ulinganifu wa fani alizoomba mwombaji, kipaumbele kwa jinsia ya kike pamoja na waombaji wenye mahitaji maalum.

‎Akizungumzia matokeo ya jumla ya uchaguzi,CPA Kasore amesema kuwa waombaji 14,433 sawa na asilimia 76 wamepangiwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi kwa ngazi ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026. Amesema kati yao wanaume ni 8,776 sawa na asilimia 61 na wanawake ni 5,657 sawa na asilimia 39.

‎Amebainisha kuwa kati ya waliochaguliwa, waombaji 12,942 wamepangiwa mafunzo ya asubuhi, huku 1,491 wakipangiwa mafunzo ya jioni. Aidha, waombaji 4,511 sawa na asilimia 24 wanasubiri kupangiwa vyuo na fani mbadala kutokana na kuchagua fani moja tu au kutokuchagua fani mbadala.

‎CPA Kasore amesema kuwa uchaguzi umefanyika katika jumla ya fani 45, ambapo fani ya Umeme imeongoza kwa kuwa na waombaji 2,980 sawa na asilimia 20.65, huku fani za Useketaji( fani ya ufundi stadi inayohusisha utengenezaji wa vitambaa kwa kutumia mashine au vifaa vya kufuma kwa mikono, maarufu kama (Handloom Weaving) na Uendeshaji wa Mitambo ( Plant Operation) zikiwa na waombaji wachache zaidi, kila moja ikiwa na waombaji watatu.

‎Aidha, Amesema kuwa VETA imepokea waombaji 134 wenye elimu ya Astashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili, ambapo 123 wamechaguliwa na 11 wanasubiri kupangiwa. Amebainisha kuwa kwa kundi hilo, baadhi ya masomo bebezi na mtambuka yameondolewa kulingana na elimu waliyonayo ili kupunguza muda wa mafunzo na kuongeza ufanisi.

‎Katika jitihada za kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali elimu, kazi au hali ya kimwili katika udahili anapata nafasi ya kujifunza , CPA Kasore amesema kuwa VETA imeondoa Mtihani wa Mchujo (Aptitude Test), hatua iliyowezesha waombaji wengi zaidi kupata fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi stadi.

‎Pia, amesema kuwa VETA imeanzisha mafunzo ya jioni katika vyuo 13, ambapo waombaji 1,491 wataanza masomo kuanzia Januari 2026, hatua inayolenga kuwahudumia wananchi waliopo kazini au wenye majukumu ya mchana.



No comments:

Post a Comment