DKT. JAFAR: "TANGAZENI HUDUMA MPYA ZA AFYA TUNAZOBORESHA KATIKA VITUO VYETU ILI WANANCHI WANUFAIKE". - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, January 5, 2026

DKT. JAFAR: "TANGAZENI HUDUMA MPYA ZA AFYA TUNAZOBORESHA KATIKA VITUO VYETU ILI WANANCHI WANUFAIKE".



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughuliki Afya, Dkt. Jafar Seif, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na Wafawidhi wote kutangaza huduma mpya za Afya zinazo ongezwa kwenye vituo vyao vya kutolea huduma ili kutoa fursa kwa jamii kutumia huduma husika.

Naibu Waziri Dkt. Jafar ametoa agizo hilo leo Januari 5, 2026 alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu katika hospitali ya Frelimo na kituo cha afya Itimba, manispaa ya Iringa mkoani humo.

Amesema Serikali imefanya maboresho makubwa hasa ya kununua vifaa tiba vya kutolea huduma mbalimbali za kibingwa, lakini sehemu kubwa ya wananchi wanaozunguka vituo husika wamesalia bila taarifa ya uwepo wa huduma hizo katika maeneo yao, na hivyo kuagiza kuwekwa kwa utaratibu rahisi na rafiki wa kuwahabarisha wananchi juu ya ongezeko la huduma mpya katika maeneo yao.

“Serikali imepeleka vifaa tiba vya kisasa ili kuboresha huduma za afya katika vituo mbalimbali, lakini wananchi wengi bado hawana taarifa za maboresho hayo. Kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, nawaagiza, tangazeni huduma mpya zinazoongezwa katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili lengo la Serikali la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi liwe na maana kwa jamii,” alisema Naibu Waziri Dkt. Seif.

Katika majumuisho ya ziara yake Dkt. Seif amewapongeza watendaji wa sekta ya afya katika ya Iringa kwa kuboresha vitengo vya huduma kwa wateja, akisema hatua hiyo inatia faraja kwa wagonjwa na kuwafanya kuwa na imani na serikali yao.

Awali Mkuu wa Sehemu za Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Manispaa ya Iringa Dkt. Godfrey Mbangali amesema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya wodi ya wazazi na wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Frelimo, kutasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na magonjwa ya dharura.



No comments:

Post a Comment