
Na, WAF-Morogoro
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo tarehe 02 Januari, 2026, ametembelea na kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya basi na lori iliyotokea usiku wa tarehe 31 Desemba, 2025 katika kijiji cha Maseyu, mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Samizi amesema hadi kufikia leo, majeruhi 5 wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, majeruhi 2 wamepewa rufaa kwenda Taasisi ya mifupa Muhimbili kwa matibabu zaidi, huku majeruhi 16 wakiruhusiwa kurejea majumbani baada ya hali zao kuimarika.
Aidha, Kuhusu marehemu, amesema kuwa miili 4 tayari imetambuliwa, ambapo miili 3 imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi. Ameongeza kuwa miili 6 ilichukuliwa vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi, na kati ya hiyo mwili 1 tayari umetambuliwa, huku ndugu wakisubiri kukamilika kwa taratibu za Kipolisi ili kuuchukua. Kwa sasa, miili 5 inaendelea kusubiri majibu ya vinasaba.
Naibu Waziri ametoa wito kwa ndugu na jamaa wa marehemu ambao bado hawajatambulika kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kusaidia zoezi la utambuzi wa miili na kukamilisha taratibu za mazishi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Samizi amesema majeruhi waliopata fursa ya kuzungumza naye wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha sekta ya afya hali iliyopelekea wao kupata huduma bora, za haraka na kwa wakati mara baada ya ajali kutokea.

Aidha, amewapongeza na kuwashukuru watendaji wa sekta ya afya kwa kujitoa kwao katika kuwahudumia majeruhi kwa wakati, huku akiwataka madereva kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari wanapotumia barabara.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, ametoa shukrani kwa Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya nchini, huku akiipongeza Wizara wa Afya, kwa kazi kubwa na usimamizi mzuri unaoendelea kufanyika katika kuhakikisha majeruhi wa ajali hiyo wanapata huduma stahiki.

No comments:
Post a Comment