Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imewataka wananchi na wateja wake kuacha mara moja tabia ya kujiunganishia huduma ya maji kinyume cha taratibu pamoja na kuingilia miundombinu ya maji, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Onyo hilo limetolewa leo Januari 28, 2026 na Afisa Mapato wa DUWASA, Bw. Fridolin Henjewele, wakati wa zoezi la ukaguzi wa miundombinu ya maji lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kubaini na kudhibiti vitendo vya hujuma na wizi wa maji.
Bw. Henjewele amesema kuwa katika zoezi hilo, DUWASA imembaini Bw. Felix Maneno, mmiliki wa yard iliyopo mkabala na Chuo cha Ufundi Stadi VETA, ambaye amejihusisha na matumizi ya maji kinyume cha utaratibu kwa kuingilia miundombinu ya mamlaka hiyo.
“Leo hii kama mlivyojionea katika eneo la tukio, tumemkamata mteja huyu ambaye alikuwa anatumia maji kinyume na utaratibu wa DUWASA. Mkaguzi wetu alipita na kugundua madhaifu haya katika miundombinu,” amesema Bw. Henjewele.
Ameongeza kuwa DUWASA haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mteja yeyote atakayebainika kutumia maji kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa, huku akitoa wito kwa wananchi wa Dodoma kushirikiana na mamlaka hiyo katika kutokomeza kabisa wizi wa maji.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Miundombinu ya Maji na Mtandao wa Maji Taka DUWASA, Bw. Alex Robert Makelemo, amesema Bw. Felix Maneno ni mteja wa muda mrefu wa DUWASA ambaye huduma yake ya maji ilisimamishwa kutokana na deni.
Amesema baada ya kusitishiwa huduma hiyo, mteja huyo aliamua kuingilia miundombinu ya maji kwa kuongeza laini nyingine ya maji ambayo haikuwa inapitia katika mfumo rasmi wa DUWASA.
“Alitoboa ukuta na kuongeza laini ya maji ya inchi moja ambayo ilikuwa inaingiza maji moja kwa moja kwenye tenki, kisha kuyatumia kwa shughuli za kuosha magari pamoja na matumizi ya walinzi wake,” amesema Bw. Makelemo.
Ameeleza kuwa mhusika tayari amepatiwa taarifa kwa njia ya simu na kuombwa kufika eneo la tukio, hata hivyo aliomba afike ofisini. DUWASA imesema imemwandikia barua ya wito ili afike ofisini kwa ajili ya majadiliano na kupatiwa gharama na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
DUWASA imeendelea kusisitiza kuwa haitavumilia vitendo vya hujuma kwa miundombinu ya maji, na itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wote kwa haki na kwa mujibu wa sheria.










No comments:
Post a Comment