
Na Anangisye Mwateba, Misenyi
Entabuko Kanyigo ambalo ni neno la Kihaya lenye maana ya Chimbuko la Kanyigo kwa lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa matamasha ya kumbukumbu yanayoelezea mambo ya kale yanayohusu kata ya Kanyigo iliyoko wilayani Misenyi katika Mkoa wa Kagera.
Lengo la tamasha hilo ambalo hufanyika tarehe 30 Disemba ya kila mwaka ni kurithisha tamaduni na naarifa ya mababu na mabibi wa Kanyigo kwa vijana wa mkoa wa Kagera hususan Kata ya Kanyigo. Tamasha hilo linahusisha kutembelea vivutio vya asili na malikale katika Kata ya Kanyigo pamoja na majadiliano namna ya kuviendeleza na kuvitumia kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika tamasha hilo Mwanzilishi na mmiliki wa Makumbusho Kata ya Kanyigo Dkt. Daniel Ndagala alisema kuwa mawazo ya kuanzisha tamasha hilo aliona ni fursa adimu kwa vijana kufahamu mambo mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa na watu wa kale lakini ni wakati mzuri wa kuwafundisha vijana fursa za kiuchumi na kijamii zinazotokana biashara ya utalii wa malikale zilizopo katika Kata ya Kanyigo.
“Sasa hivi tunaimba wimbo wa kufikisha watalii milioni nane ifikapo 2030, lakini tuko watanzania milioni 60, watanzania hatuna tabia ya kutembelea vivutio vyetu vya utalii. Hakuna mtalii wa nje anakuja kugawa fedha tu kama njugu watalii wa nje wanapokuja ni fursa muhimu kwa watanzania kuendeleza faida za mnyororo wa utalii kama vile kutoa huduma za malazi, chakula, kuuza bidhaa mbalimbali za kiutamaduni hivyo ni vema tutumie fursa za kutangaza maeneo yetu ili tupate watalii wa ndani na nje” alisema Dkt. Ndagala
Kwa upande wa Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Malikale na Mkumbusho Bw. William Mwita alisema kuwa kupitia sheria ya mambo ya Malikale ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2022, Wizara ya Maliasili na Utalii iliruhusu sekta binafsi kuanzisha na kumiliki makumbusho pamoja na maeneo ya malikale kwa faida ya kijamii na kiuchumi.
Bw. Mwita aliongeza kuwa jukumu la wizara ni kutoa miongozo ya namna bora ya kuendesha makumbusho hayo pamoja na usimamizi wa maeneo ya malikale kama ambavyo wanafanya kwa makumbusho ya Kanyigo pamoja na Tamasha la Entabuko.
“Uanzishwaji wa makumbusho, matamasha ya kumbukumbu na uendeshaji wa maeneo ya malikale unaofanywa na sekta binafsi unalenga kutengeneza fursa za ajira kupitia utalii wa malikale ambapo mpaka sasa yako makumbusho binafsi takribab 42 nchi nzima” alisema Bwana Mwita.




No comments:
Post a Comment