
Na Andrew Mbai - Zanzibar
Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA CPA (T) Musa Nassoro Kuji pamoja na Bingwa wa medali ya dhahabu wa mbio ndefu za Dunia 2025 Alphonce Simbu jana tarehe 31.12.2025 walipokelewa kwa heshima Zanzibar kufuatia mwaliko maalum kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwaliko huo maalum kwa TANAPA na Bingwa wa Dunia wa Mbio ndefu zilizofanyika mwaka 2025 Tokyo Japan Alphonce Simbu, ni kwa ajili ya wao kushiriki katika Bonanza maalum la mazoezi ya viungo Zanzibar kwa mwaka 2026 lililofanyika asubuhi ya leo tarehe 01.01.2026 Mjini Zanzibar lililoanza kwa matembezi.
Matembezi hayo yaliongozwa na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambayo yalianzia katika eneo la Michenzani hadi katika Uwanja wa ”New Amani Complex” uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Katika kuhitimisha bonanza hilo, mwanariadha na bingwa wa dunia wa mbio ndefu zilizofanyika mwaka 2025 Jijini Tokyo Japan, Alphonce Simbu alipata nafasi ya kutambulishwa kwa wana mazoezi waliohudhuria bonanza hilo na kupiga picha na mhe. Rais wa Zanzibar.
Naye Kamishna Kuji akiongea baada ya kukamilika kwa bonanza hilo alimshukuru Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaliko maalum kwa TANAPA pamoja na mwanariadha bingwa wa dunia wa mbio ndefu kwani ziara hiyo ya pamoja kati ya TANAPA na mwanariadha huyo itatoa hamasa kwa vijana wanariadha waliopo Zanzibar kupata hamasa ya kuweka nia nao kuja kuwa wanariadha bora kama Simbu.
“Kipekee ninamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoipa kipaumbele sekta ya utalii pamoja na michezo nchini ambapo jitihada hizo zimepelekea kukua kwa vipaji vya wanamichezo wanaofanya vizuri duniani kama alivyofanya Alphonce Simbu. Pili, ninamshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaliko huu maalum ambao umewezesha TANAPA kushiriki kwenye bonanza maalum kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 62 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar” ~ alisema Kamishna Kuji.
Naye Mwana riadha Alphonce Simbu ameishukuru TANAPA kwa kumuwezesha kukanyaga ardhi ya Zanzibar kwa mara ya kwanza na ameahidi kuendelea kukuza kipaji chake ili kupitia ushindi wake aendelee kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa Tanzania pamoja na nchi ya Tanzania kwa ujumla.
Akiwahutubia washiriki wa bonanza hilo lililohudhuriwa na washiriki zaidi ya 500 kutoka vikundi 165 vya mazoezi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zainzar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliwapongeza washiriki wote kwa ushiriki wao na kujituma katika kufanya mazoezi.
“Michezo ni nguzo muhimu katika kuimarisha afya pamoja na kuleta umoja na mshikamano na hatimaye kuendelea kudumisha amani na kuwa na afya njema. Tutaendelea kuboresha miundombinu ya michezo yote ili Zanzibar iwe kitovu cha utalii wa michezo” ~ alisema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Utalii wa michezo ni zao jipya la utalii ambalo linahitaji kuendelea kuwekewa msukumo, uwezeshwaji na uboreshwaji wa miundombinu yake ili kuwavutia wana michezo wengi zaidi ambao watashiriki katika michezo hiyo na kupata ushindi kitaifa na kimataifa na hatimaye kuitangaza Tanzania na kuvutia watalii wengi kuja kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini.
Bonanza la mazoezi ya viungo Zanzibar 2026 limeandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar wakishirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar pamoja na Chama cha Mchezo wa Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) lenye kauli mbiu “amani na mshikamano wetu, ni tunu ya Taifa letu”.



No comments:
Post a Comment