
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, (Kushoto) na Mkurugenzi wa Shirika la LSF, Lulu Ng’wanakilala (kulia) wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Shirika la Legal Services Facility (LSF)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, (Kushoto ) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Razack Lokina (kulia), wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Chuo Kikuu cha Dodoma, Januari 8,2026.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, (Kushoto) na Mkurugenzi wa Shirika la LSF, Lulu Ng’wanakilala (kulia ) wakikabidhiana makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Shirika la Legal Services Facility (LSF) baada ya kusainiwa Januari 8,2026 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shirika la Legal Services Facility (LSF) iliyofanyika Januari 8,2026 jijini Dodoma.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Razack Lokina,akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shirika la Legal Services Facility (LSF), iliyofanyika Januari 8,2026 jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Shirika la LSF, Lulu Ng’wanakilala,akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shirika la Legal Services Facility (LSF) iliyofanyika January 8,2026 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema huduma ya msaada wa kisheria si fadhila wala hisani, bali ni haki ya msingi ya kila Mtanzania isiyotenganishwa na misingi ya Katiba, utawala bora na wajibu wa dola kwa wananchi wake.
Maswi ameyasema hayo leo Januari 8,2026 jijini Dodoma, wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shirika la Legal Services Facility (LSF) yanayotarajiwa kuleta manufaa makubwa katika kuboresha na kupanua upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi nchini
Ambapo Maswi amekiri kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, bado zipo changamoto za kimuundo zinazokwamisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wengi.
Amesema ukweli uliopo ni kwamba wananchi wengi, hususan wa kipato cha chini, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na wanaoishi maeneo ya pembezoni, wamekuwa wakikosa haki zao si kwa sababu hawana hoja au ushahidi, bali kutokana na kushindwa kugharamia mifumo ya kisheria ya kuzipigania haki hizo.
Maswi ameeleza kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni bado hawafikiwi ipasavyo na huduma za haki kutokana na uhaba wa miundombinu, rasilimali watu, vitendea kazi pamoja na ofisi za watoa huduma za kisheria.
“Changamoto hizi haziwezi kupuuzwa wala kuachwa ziendelee. Zinahitaji majibu ya kimkakati, hatua za makusudi na ushirikiano wa kina wa kitaasisi. Ndiyo maana makubaliano haya tuliyosaini leo ni hatua ya makusudi ya Serikali ya kupanua wigo wa haki, kupeleka huduma karibu na wananchi, kuvunja vikwazo vya kijiografia na kijamii na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyokubalika,” alisema Maswi.
Amesema kupitia makubaliano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Chuo Kikuu cha Dodoma, pande hizo zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya msingi na ya kimkakati, ikiwemo utoaji wa elimu ya kisheria kwa wananchi, kufanya tafiti za kina kuhusu upatikanaji wa haki, pamoja na kuanzisha na kuendesha Kituo cha Pamoja cha Huduma za Msaada wa Kisheria katika ngazi ya Mkoa.
Maswi amesema kituo hicho kitakuwa mhimili muhimu wa utoaji wa huduma jumuishi, kikitoa uwakilishi wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu mawakili binafsi, pamoja na kuwa kituo cha rufaa kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma.
“Huu ni mfano halisi wa utekelezaji wa sera kwa vitendo—sera inayoshuka kutoka kwenye maandiko kwenda moja kwa moja kwa mwananchi,” amesema.
Kwa upande wa Shirika la LSF, Maswi alisema makubaliano hayo yanalenga kuimarisha kwa kiwango kikubwa mfumo wa Wasaidizi wa Kisheria nchini, hatua itakayohusisha uwekezaji wa makusudi katika mafunzo endelevu, vitendea kazi, miundombinu ya ofisi, usafiri na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi, kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kitaifa.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utafanyika kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha za umma.
“Ni dhamira thabiti ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi. Ushirikiano huu ni ushahidi wa vitendo wa falsafa ya Haki kwa Wote, na ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga taifa linalozingatia misingi ya haki, usawa, uwajibikaji na utawala wa sheria,” amesema Maswi.
Amesema pia Wizara itasimamia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa dhati, kwa uwazi na kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya uwajibikaji wa umma, huku Serikali ikiendelea kufuatilia, kutathmini na kuboresha utekelezaji wa ushirikiano huo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la LSF, Lulu Ng’wanakilala, amesema upatikanaji wa haki ni haki ya kikatiba na msingi wa utawala bora, akiongeza kuwa bila mifumo imara na endelevu ya msaada wa kisheria, haki hiyo hubaki kuwa ndoto kwa wananchi wengi.
Amesema kwa mwaka huu, ajenda ya uendelevu wa huduma za msaada wa kisheria ndiyo kipaumbele kikuu cha LSF, na kupitia hati hiyo ya makubaliano, shirika hilo linaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuunga mkono jitihada za Wizara katika elimu ya sheria kwa umma, tafiti, mijadala ya kitaifa pamoja na uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya uendelevu wa huduma za msaada wa kisheria.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Razack Lokina, alisema ushirikiano huo unaimarisha nafasi ya UDOM kama mshirika wa kimkakati wa Serikali katika kutekeleza ajenda za haki, utawala bora na maendeleo ya jamii.
Amesema ushirikiano huo utaimarisha wigo wa huduma za msaada wa sheria kwa wananchi, hususan makundi yenye uhitaji maalumu kama wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wananchi wasio na uwezo wa kifedha, sambamba na kukuza uelewa wa Katiba na sheria ndani ya jamii.
Profesa Lokina ameongeza kuwa hatua hiyo itaimarisha umahiri wa wanafunzi wa sheria kwa vitendo, kuzalisha wanasheria mahiri, waadilifu na wenye mtazamo wa kuhudumia jamii tangu wakiwa vyuoni, kuongeza ufanisi wa utawala wa sheria nchini na kupunguza wingi wa kesi kwenye vyombo vya utoaji haki.






No comments:
Post a Comment