‎PROF. KUSILUKA ASISITIZA TAFITI SHIRIKISHI KUKABILI CHANGAMOTO ZA AFYA YA AKILI KWA VIJANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 6, 2026

‎PROF. KUSILUKA ASISITIZA TAFITI SHIRIKISHI KUKABILI CHANGAMOTO ZA AFYA YA AKILI KWA VIJANA



‎Na. Meleka Kulwa- Dodoma.


‎Katika hatua inayotajwa kuwa mwanga mpya kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimezindua rasmi mradi wa u’GOOD TevuAfya, unaolenga kushughulikia kwa vitendo matatizo ya afya ya akili kwa vijana, hususan wanaoishi mijini na pembezoni mwa miji.

‎Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Januari 6, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Afrika Mashariki, ukihusisha viongozi wa chuo, watafiti, wadau wa maendeleo pamoja na wanafunzi.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka, amesema mradi wa u’GOOD TevuAfya ni miongoni mwa miradi 23 ya kimataifa inayotekelezwa chini ya programu ya Good Life, huku miradi minane ikitekelezwa Tanzania.

‎“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Tanzania inaendelea kujijengea heshima na nafasi muhimu katika ramani ya utafiti wa kisayansi duniani,” amesema Profesa Kusiluka.

‎Ameeleza kuwa ushindani wa kupata ufadhili wa miradi ya utafiti ni mkali, hivyo mafanikio ya watafiti wa Tanzania kupata miradi hiyo yanaonesha ubora wa kazi na umuhimu wa tafiti zinazolenga kutatua matatizo halisi ya jamii.

‎Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, changamoto za afya ya akili kwa vijana zimeongezeka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo hali ngumu za kiuchumi, mabadiliko ya mifumo ya kifamilia, msongo wa mawazo, matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii pamoja na kasi ya maendeleo ya teknolojia za kidijitali.

‎“Afya ya akili si tatizo la vijana pekee, ni suala la jamii nzima. Familia, wazazi na mazingira yanayowazunguka vijana vina mchango mkubwa,” amesema, akisisitiza umuhimu wa tafiti shirikishi zitakazosaidia kupata suluhisho endelevu.

‎Aidha, ametoa wito wa kuimarishwa kwa elimu ya uraia kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujiamini na kuiona Tanzania kama nchi ya fursa na matumaini, akibainisha kuwa misingi ya maadili na utambulisho wa kitaifa ina mchango mkubwa katika ustawi wa afya ya akili.

‎Kwa upande wa wanafunzi, Akley Omary wa UDOM amesema afya ya akili ni uwezo wa mtu kukabiliana na mawazo chanya na hasi yanayotokana na changamoto za maisha na mazingira ya kijamii.

‎Amesema wanafunzi wengi hukumbwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za kifedha, matatizo ya kifamilia na mazingira magumu ya masomo, huku kukosa mahitaji muhimu kama chakula, vifaa vya masomo na fedha za matumizi vikizidi kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia.

‎Naye David Julius, mwanafunzi wa Shahada ya Business Information System, amesema dhana potofu kwamba afya ya akili ni sawa na wazimu imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana kutafuta msaada.

‎“Afya ya akili ni uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi na kuchanganua mambo kwa ufanisi, kufeli masomo na kushindwa kufanya maamuzi sahihi mara nyingi hutokana na msongo wa mawazo,” amesema.

‎Kwa upande wake, Rebeca Omari Kabanda, mwanafunzi wa Information Security Engineering, amesema ukosefu wa ajira ni moja ya changamoto kubwa zinazowaathiri vijana kisaikolojia, hasa pale matarajio ya maisha baada ya kuhitimu yanapogonga mwamba.

‎Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA na mitandao ya kijamii yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa kujiepusha na tabia hatarishi na mahusiano yasiyo rasmi yanayoweza kuathiri afya ya akili na maendeleo ya kielimu.

‎Mradi wa u’GOOD TevuAfya unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera pamoja na mbinu za vitendo zitakazosaidia kuboresha afya ya akili kwa vijana na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wenye afya njema ya mwili na akili.


No comments:

Post a Comment