SERIKALI YAIMARISHA MAZINGIRA WEZESHI KWA UTOAJI WA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 28, 2026

SERIKALI YAIMARISHA MAZINGIRA WEZESHI KWA UTOAJI WA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA NCHINI



Na Mwandishi Wetu - ARUSHA


Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mawakili wa Serikali na taasisi zote zinazotoa huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia Watanzania wote kwa usawa, haki na ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb.), katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amosi Makalla, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria kuhusu utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, yanayofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Januari, 2026 jijini Arusha.

Katika hotuba hiyo, Dkt. Homera amesema Serikali inaendelea kutekeleza dhamira ya kuhakikisha wananchi wote, hususan wanyonge na walioko maeneo ya pembezoni, wanapata huduma za msaada wa kisheria kwa wakati na kwa ufanisi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosisitiza haki, usawa na ustawi wa wananchi wote.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, kuimarisha uendelevu wa huduma hizo pamoja na kuongeza ufanisi katika kusimamia na kutetea haki za wananchi.

Amesisitiza kuwa Mawakili wa Serikali ni nguzo muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na mfumo wa utoaji haki nchini.

Aidha, Waziri Homera amebainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ina mpango wa kuwawezesha Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria wenye sifa za kuwa Mawakili wa Kujitegemea kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, ikiwemo uwakilishi wa mashauri yasiyo na mgongano wa kimaslahi na waajiri wao. Hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya watoa huduma za msaada wa kisheria na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko vijijini na maeneo ya mbali.

Vilevile, amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia taaluma yao kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya redio jamii, mikutano ya kijamii, warsha na makundi ya kijamii kama bodaboda na mama lishe, kwa lengo la kuongeza uelewa wa haki na wajibu wa wananchi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika jamii.

Akizungumzia changamoto za kijamii, Waziri Homera amesema bado kuna malalamiko mengi ya wanawake, watoto na makundi maalum kunyimwa haki zao kutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Hivyo, amewataka Mawakili wa Serikali kuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii kuachana na mifumo kandamizi na kuhamasisha wananchi kuandika wosia ili kulinda haki za familia, wajane na watoto.

Mafunzo hayo yanahusisha Mawakili wa Serikali kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Maafisa Sheria, na yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuboresha mfumo wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wananchi.







No comments:

Post a Comment