SERIKALI YAWAASA WAZAZI KUWAPELEKA SHULE WATOTO WAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 13, 2026

SERIKALI YAWAASA WAZAZI KUWAPELEKA SHULE WATOTO WAO



Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa amesema ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya elimu bora katika mazingira salama na rafiki kwa ujifunzaji.

Mhe. Kwagilwa ameyasema hayo Januari 12, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Utili, Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Utiri – Mahande, ambapo aliwakumbusha wananchi kuhusu wajibu wao katika kutimiza haki ya mtoto kupata elimu.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kwagilwa ameagiza ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea kukamilishwa haraka, akisisitiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kukosa darasa au kusoma katika mazingira duni ilhali Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya miundombinu ya elimu.

“Asiwepo mtoto akabaki nyumbani bila kupelekwa shule, ilhali sisi Serikali tumeshaweka mazingira mazuri na Mheshimiwa Rais ameweka miundombinu yote. Tuko tayari kuwapokea watoto wetu, waleteni watoto wadogo waje wapate haki yao,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kushirikiana na Serikali kuhakikisha kila mtoto anahudhuria masomo bila kikwazo, akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Kwagilwa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya elimu, ili kuhakikisha ubora, thamani ya fedha na matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya Watanzania.



No comments:

Post a Comment