Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amebainisha mikakati ya muda mfupi inayotekelezwa na Serikali ili kupunguza changamoto ya foleni katika barabara ya Kibaha–Chalinze hadi Morogoro.
Ulega amesema hayo leo tarehe 28, Januari 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Pwani Mhe. Hawa Mchafu aliyehoji hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya njia nane pamoja na mikakati ya muda mfupi ya kuondoa foleni katika barabara hiyo.
Ulega amesema mikakati hiyo ni pamoja na kujenga upya barabara ya zamani iliyokuwa ikitumika kabla ya kujengwa barabara ya Kibaha–Chalinze, ambayo kwa sasa imeelemewa na msongamano mkubwa wa magari.
Aidha, Ulega amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuondoa foleni zinazotokana na magari yanayoharibika barabarani.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kibaha–Chalinze hadi Morogoro, Waziri Ulega amesema mradi huo uko katika hatua za awali, huku Serikali ikitangaza upya zabuni baada ya kutofautiana na mkandarasi wa awali.
Ameongeza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi mpya uko katika hatua nzuri.


No comments:
Post a Comment