SITAVUMILIA UZEMBE WOWOTE UTAKAOKWAMISHA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE - MCHENGERWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 15, 2026

SITAVUMILIA UZEMBE WOWOTE UTAKAOKWAMISHA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE - MCHENGERWA

 

Na Mwandishi Wetu - Dodoma 


Katika kuhakikisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatekelezwa ipasavyo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hatovumilia mazoea au uzembe wowote utakaokwamisha utekelezaji wa mabadiliko hayo muhimu kwa wananchi.


Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Januari 14,2026 Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya pamoja na watumishi wa sekta ya afya wa Mkoa wa Dodoma. Kikao hicho kimefanyika katika viwanja vya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

‎Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amesema kuwa utoaji wa huduma bora za afya ni msingi wa heshima ya maisha ya binadamu na haupaswi kuathiriwa na uzembe, ucheleweshaji wa maamuzi au udhaifu wa mifumo ya uendeshaji wa hospitali.‎


‎"Wananchi wanaofika hospitalini wanapaswa kupata huduma bora bila visingizio, hivyo imani ya mwananchi kwa mfumo wa afya hujengwa na kuvunjwa kupitia namna huduma inavyotolewa,"amesema. 


‎Aidha, Waziri mchengerwa amesisitiza umuhimu wa hospitali kuzingatia taratibu zilizoandikwa na zinazofuatwa, pamoja na kupima matokeo ya huduma zinazotolewa ili kubaini mapungufu na kuyarekebisha kwa wakati. Amebainisha kuwa kujifunza kutokana na makosa na kulinda usalama wa wagonjwa na wahudumu ni sehemu muhimu ya utoaji wa huduma bora.

‎Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi tangu kuanzishwa kwake.


"Katika kipindi cha miaka kumi, hospitali yetu imeanzisha huduma za kibingwa 20 na 18 zikiwa za kibobezi (ubingwa wa Juu)  ,huku asilimia 60 ya huduma hizo zikianzishwa ndani ya miaka Minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,"amesema. 


‎Ametaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni pamoja na upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto, upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima, uchunguzi na uzibaji wa mishipa ya moyo, radiolojia ya kimataifa, uvunjaji wa mawe kwa mawimbi, matibabu ya homoni, magonjwa ya mfumo wa chakula, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, upasuaji wa mifupa ikiwemo nyonga na magoti, pamoja na huduma za utalii wa matibabu na uchunguzi wa afya ya kina.


‎Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya na dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za kibingwa kwa wananchi ndani ya nchi.‎

No comments:

Post a Comment