WATOA HUDUMA KWA MANUSURA WA VITENDO VYA UKATILI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA JAMII. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 9, 2026

WATOA HUDUMA KWA MANUSURA WA VITENDO VYA UKATILI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA JAMII.


Na Abdala Sifi WMJJWM – Dodoma.


Wadau wanaotekeleza eneo namba sita la Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) wametakiwa kuunganisha nguvu kuhakikisha huduma hizo zinafahamika kwa jamii ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa manusura.

Hayo yamesemwa tarehe 09 Januari 2026, Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdnoor wakati kikao kilichokutanisha Wizara za Kisekta, Idara za Serikali, Asasi za Kiraia, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wa maendeleo kwa lengo la kupokea taarifa na kujadili mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuratibu huduma hizo.  

Mkurugenzi Badru ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu, amesema wadau wana nafasi kubwa ya kusaidia Serikali katika kuhamasisha jamii, kujenga imani kwa mifumo ya huduma na kuhakikisha hakuna manusura anayebaki nyuma kwa kukosa taarifa au msaada.

“Niwaombe wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuanzisha na kutekeleza programu za kisera na kijamii zinazolenga kuzuia ukatili, kubadili mitazamo hasi na kuimarisha mwitikio wa Kitaifa dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto nchini”.

Aidha amesema kwa utafiti wa Kitaifa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo mwaka 2024, kuhusu ukatili dhidi ya watoto na vijana walio kati ya umri wa miaka 13-24, ulibainisha hali halisi ya ukatili, ambapo asilimia 16.4 ya wasichana na asilimia 31.1 ya wavulana ambao walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono walifahamu uwepo wa huduma za manusura wa vitendo hivyo jambo ambalo linadhihirisha uhitaji wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa wadau kutoka Shirika la UN Women Godlizan Bakary amesema mwamko kwa jamii unaeendelea kuongezeka kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na kwamba wadau wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili zinafahamika vyema kwa jamii na kuzitumia ipasavyo.

No comments:

Post a Comment