Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu, kufuatia operesheni maalumu zilizofanyika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2025, katika mikoa mbalimbali nchini.
Katika operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 66 walikamatwa kuhusiana na uhalifu wa biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wananchi pamoja na uimarishaji wa mikakati ya kiintelijensia katika kudhibiti mitandao ya dawa za kulevya.
Katika operesheni iliyofanyika eneo la Sinza C, mtaa wa Bustani, nyumba namba 16, jijini Dar es Salaam, mamlaka ilimkamata Jefferson Kilonzo Mwende (35), raia wa Kenya, akiwa na gramu 131.88 za heroin. Uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiishi nchini tangu mwaka 2023 na alitumia biashara ya kuuza chai kama kivuli cha kuficha shughuli zake za kuuza dawa za kulevya.
Aidha, katika mtaa wa Wailes, Temeke, Dar es Salaam, DCEA ilifanikiwa kukamata pakiti 20 za skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03, zilizokuwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba na kusafirishwa kwa kutumia basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili za Msumbiji AAM 297 CA. Basi hilo hufanya safari zake kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania.
Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam, pamoja na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji.
Katika tukio jingine lililotokea eneo la Kinyerezi, mtaa wa Majoka wilayani Ilala, watuhumiwa Erick Ernest Ndagwa (32), Paul Blass Henry (34) na Tido Emmanuel Mkude (35) walikamatwa wakiwa na bangi yenye uzito wa kilogramu 193.66, iliyokuwa ikisafirishwa kutoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Kadhalika, ukaguzi uliofanyika kwenye kampuni za usafirishaji wa mizigo jijini Dar es Salaam ulisababisha kukamatwa kwa pakiti 20 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54, zilizokuwa zimefungwa na kutambulishwa kama majani ya mwarobaini yaliyokaushwa. Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kutoka Kenya kuelekea Australia.
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, kupitia operesheni mbalimbali zilizofanyika katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Tanga, Lindi, Kilimanjaro, Njombe, Kigoma na Arusha, mamlaka ilikamata heroin gramu 37.34, skanka kilogramu 1.015, bangi kilogramu 7,969.98 na mirungi kilogramu 1,363.701, pamoja na kuteketeza ekari 14 za mashamba ya bangi.
DCEA imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za viashiria vya biashara ya dawa za kulevya, sambamba na kuwa makini kutojiruhusu kusafirisha mizigo wasiyoifahamu.












No comments:
Post a Comment