
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yoichi Mikami na kujadiliana naye masuala ya uchumi, miradi ya maendeleo na uwekezaji.
Akizungumza na Balozi huyo leo (Jumatano, Januari 14, 2026) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Mkuu ameishukuru nchi hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali kama vile barabara ya Arusha hadi Holili, bandari ya Kigoma, miradi ya kilimo na upatikanaji wa vifaa tiba vya huduma za afya ya mama na mtoto.
“Serikali itahakikisha kuwa miradi hii inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na inakamilishwa kama ilivyopangwa,” amesema Dkt. Mwigulu
Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kutuma salamu za pongezi kwa Waziri Mkuu wa Japan, Bibi Sanae Takaichi kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo tangu Oktoba, 2025 na kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo. “Tanzania inasisitiza kuendeleza ushirikiano wa karibu na Japan kwa manufaa ya pande zote mbili,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi Mikami alimweleza Waziri Mkuu kwamba amefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kijamii 79 ambayo awali ilikuwa inasuasua na kwamba tangu Septemba, 2024 hadi sasa, imebakia miradi 16 tu.
Alisema nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa miaka zaidi ya 60.



No comments:
Post a Comment