Balozi wa Singapore nchini Tanzania mwenye makazi jijini Singapore, Mhe. Douglas Foo amewasili nchini Februari 22, 2026 kwa ziara ya kikazi ya siku sita kuanzia tarehe 22 hadi 27 Februari, 2026.
Lengo la ziara yake ni kuimarisha ushirikiano wa uwili baina ya Tanzania na Singapore katika maeneo yenye maslahi kwa pande hizi mbili ikiwemo biashara, uwekezaji na kubadilishana utaalam katika nyanja mbalimbali kama vile usimamizi wa bandari, utawala bora, mipango miji na maendeleo ya viwanda.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Balozi Foo ambaye ameambatana na Afisa Dawati anayeshughulikia masuala ya Asia Kusini na Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Singapore, Bi. Desiree Wee Zhi Yi, alipokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Dkt. Luangisa Emmanuel Francis.
Vilevile, Mhe. Balozi Foo alipata fursa ya kusalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo ambaye alikuwa Uwanjani hapo akiwa njiani kuelekea Mkoani Songwe kwa majukumu mengine ya kikazi mkoani humo. Mhe. Waziri Kombo alikuwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Lt. Jen (Mst.), Yacoub Mohamed.
Akiwa nchini, Mhe. Balozi Foo atakutana na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Sekta Binafsi kwa ajili ya kujadiliana nao juu ya umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.





No comments:
Post a Comment